Theresia Gasper – Dar es Salaam
BAADA ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons, uongozi wa Azam FC, umepanga kutorudia makosa katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC ya Kinondoni unaotarajiwa kuchezwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hiyo ni sare ya pili mfululizo kwa Azam baada ya ile ya kwanza dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa Azam FC, Jafar Idd, alisema makosa waliyofanya mwishoni wa mchezo yamewagharimu na kulazimishwa sare.
“Huu ni mchezo wa pili mfululizo kupata sare, kwa sasa tunajiandaa kukutana na KMC Jumamosi hii, tutahakikisha tunakuwa makini ili tusifanye makosa yoyote ambayo yanaweza kutugharimu,” alisema.
Alisema baada ya mchezo wa juzi, kikosi hicho kiliingia kambini kuendelea na maandalizi ya mechi ijayo, ikiwa ni pamoja na kuyafanyia kazi kasoro zilizojitokeza. Azam inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo, ikijikusanyia pointi 38 kati ya mechi 19 walizocheza, wakishinda 11, sare tano na kupoteza tatu.