NA WINFRIDA NGONYANI, DAR ES SALAAM
RAIS wa klabu ya soka ya Simba, Evance Aveva, ametamba timu hiyo itapata mafanikio makubwa katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao kutokana na usajili utakaofanywa.
Simba bado haijaweka wazi mikakati yao ya usajili kwa kuanika majina ya wachezaji wanaowataka ikiwemo watakaoachwa baada ya mikataba yao kumalizika na wengine ambao viwango vyao vimeshuka.
Wekundu hao wa Msimbazi waliomaliza nafasi ya tatu katika michuano ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita, juzi walifanikiwa kunasa saini ya kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohamed Ibrahim na kumsainisha mkataba wa miaka miwili ili kukiboresha kikosi.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Aveva aliwataka wanachama na wapenzi wa klabu ya Simba kuendelea kuiombea dua timu hiyo kwani uongozi upo makini kuhakikisha wanasajili wachezaji watakaofanya vizuri na kurudisha heshima ya timu hiyo.
Usajili wa Ibrahim umefanya idadi ya wachezaji waliosajiliwa Simba hadi sasa kufikia watano wengine wakiwa ni Muzamir Yassin (Mtibwa Sugar) Jamal Mnyate, Emmanuel Semwanza (wote Mwadui FC) na Hamad Juma (Coastal Union).
“Usajili tunaofanya sasa ni sehemu ya kurekebisha kikosi chetu ambacho kilimaliza katika nafasi ya tatu msimu uliopita, ambapo mahasimu wetu Yanga walitetea taji lao la ubingwa huku Azam FC wakimaliza nafasi ya pili,” alisema.
Alisema Simba ipo mbioni kupata kocha mpya ambaye atakinoa kikosi hicho msimu ujao.
Simba imekuwa na wakati mgumu katika ushiriki wake Ligi Kuu Bara kutokana na kushindwa kunyakua ubingwa huo tangu msimu wa 2011/12 hali iliyowanyima fursa ya kushiriki michuano ya kimataifa licha ya kubadilisha makocha mara kwa mara.