Umoja wa Afrika (AU) pamoja na Umoja wa Mataifa (UN) wanaunga mkono serikali ya kiraia nchini Sudan baada ya kupinduliwa madarakani kwa rais Omar al-Bashir mwezi uliopita.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat, amesema kwamba hatua ya baraza la jeshi kuendelea kuongoza nchi hiyo ni jambo lisilokubalika.
Mahamat ameyasema hayo baada ya kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Mkuu huyo wa Umoja wa Afrika lakini amesema kwamba wanajeshi wanaweza kuwa sehemu ya serikali ya kiraia.
Waandamanaji wameendelea kushinikiza kwamba wanataka serikali ya kiraia na Umoja wa Afrika awali ulilipa jeshi la Sudan muda wa mwisho wa siku kumi na tano kupeana madaraka kwa raia, ingawa muda huo uliongezwa hadi siku sitini.