MASOKO ya fedha na hisa duniani yana wasiwasi mkubwa. Juni 23 mwaka huu Waingereza watapiga kura ya maoni kuamua nchi yao iendelee kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ulaya au ijitoe. Ikiwa wapiga kura wa Uingereza wataamua kujitoa, paundi ya Uingereza itaporomoka, thamani za hisa zitapungua katika masoko ulimwenguni kote, pia kuna uwezekano wa mtikisiko wa uchumi wa duniani.
Mpaka naandika makala hii, sampuli za kura za maoni zinaonyesha kuwa wanaotaka kujitoa watashinda.
SABABU YA KURA YA MAONI
Baadhi ya viongozi wa Chama cha Wahafidhina (Conservative) na wanachama wao wanaamini Jumuiya ya Ulaya inapunguza uhuru wa dola ya Uingereza kuamua mambo yake yenyewe.
Uingereza inalipa mchango mkubwa kwenye Jumuiya ya Ulaya kuliko matumizi ya Jumuiya ya Ulaya nchini Uingereza. Kwa mfano mwaka 2015 Uingereza ilichangia paundi bilioni 12.9 sawa na wastani wa paundi 200 (Sh 600,000) kwa kila Muingereza.
Matumizi ya Jumuiya ya Ulaya nchini Uingereza yalikuwa paundi bilioni 5.8, mchango halisi wa Uingereza ni paundi bilioni 7.1. Wanaotaka kujitoa wanadai fedha hizi zinaweza kutumiwa vizuri nchini Uingereza.
Wanaopinga Uingereza kuendela kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ulaya wanaona nchi yao inaathirika na uhamiaji mkubwa kutoka nchi za nje. Mwaka 2015 Uingereza ilipokea wahamiaji zaidi ya 330,000 nusu yao wakitokea nchi za Ulaya Mashariki.
Wahamiaji wanaongeza ushindani katika soko la ajira na kusababisha kutoongezeka kwa mishahara ya chini. Wanatumia huduma za afya za taifa lakini pia wanachangia katika mfuko unaogharamia huduma hizo. Wanaotaka kujitoa wanadai kuwa malipo ya hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi wahamiaji kutoka nchi nyingine za Jumuiya ya Ulaya hasa nchi za Ulaya Mashariki – Poland, Hungary, Slovakia na Jamhuri ya Czech ni mzigo mkubwa.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, David Cameron alifanya mazungumzo na Jumuiya ya Ulaya ili Uingereza isiwajibike katika baadhi ya sera za Jumuiya ya Ulaya hasa lengo la Jumuiya hiyo kuunda Shirikisho la Ulaya.
Uingereza si mwanachama wa Umoja wa Sarafu ya Ulaya – Eurozone. Inatumia sarafu yake ya paundi. Uingereza ilitaka ilindwe na isiwajibike kutekeleza maamuzi yanayofanywa na umoja wa sarafu na hususan Benki Kuu ya Ulaya.
Jumuiya ya Ulaya iliikubalia Uingereza kuwa hailazimiki kutekeleza lengo la ushirikiano wa karibu wa wananchi wa nchi za Ulaya. Suala hili liliishaamuliwa na Jumuiya ya Ulaya tangu mwaka 2014. Kimsingi Jumuiya ya Ulaya ilifikia makubaliano ya kumuondolea aibu Waziri Mkuu, David Cameron kumuwezesha kuwaeleza Waingereza kuwa Jumuiya ya Ulaya imekubaliana na matakwa ya Uingereza. Baadhi ya Viongozi wa chama chake wakiwemo mawaziri hawakukubali kuwa amefanikiwa kupata mambo muhimu waliyoyataka na hasa suala la kuzuia wahamiaji wasiingie kwa wingi Uingereza.
Katika kampeni yao, wanaotaka kujitoa wanadai kuwa Uturuki imo ndani ya mchakato wa kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ulaya. Itakapojiunga na Jumuiya ya Ulaya, wahamiaji wengi toka Uturuki wataenda Uingereza kutafuta kazi. Kwa kuwa Waturuki ni Waislam, hilo litakuwa tukio la kuhatarisha usalama wa Uingereza. Ukweli ni kwamba Jumuiya ya Ulaya haina nia ya kuikubalia Uturuki ijiunge na Jumuiya hiyo. Lakini viongozi wa kambi ya kujitoa toka Jumuiya ya Ulaya wametumia vizuri propaganda ya tishio la wahamiaji kutoka Uturuki kuvutia Waingereza waikatae Jumuiya ya Ulaya.
Wanaotaka kujiondoa toka Jumuiya ya Ulaya wanaongozwa na Boris Johnson, Meya wa London 2008 – 16, na ambaye hivi sasa ni Mbunge katika Bunge la Uingereza. Baraza la Mawaziri la David Cameron limegawanyika. Kuna baadhi ya Mawaziri wanafanya kampeni kupinga Uingereza kuendelea kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ulaya.
Wanaotaka kujiondoa toka Jumuiya ya Ulaya wanadai kuwa urasimu wa Jumuiya ya Ulaya unazuia uwekezaji katika shughuli za uchumi nchini Uingereza na unainyima fursa nchi hiyo kukuza biashara na nchi nyingine kama vile China na India.
ATHARI ZA KUJIONDOA
Utafiti wa taasisi mbalimbali likiwemo Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo  (OECD) na vyuo vikuu unaonyesha kuwa Uingereza itaumia kiuchumi ikiwa itapiga kura kujiondoa Jumuiya ya Ulaya. Kujiondoa katika Jumuiya ya Ulaya kutapunguza biashara ya kimataifa, uwekezaji kutoka nje na ukuaji wa uchumi, utapunguza ajira na hali ya maisha ya Waingereza. Ikiwa Uingereza itajitoa, biashara ya kimataifa na nchi za Jumuiya ya Ulaya inaweza kupungua kwa asilimia 10 ya pato la taifa na uwekezaji kutoka nje utapungua kwa asilimia 3.4.
Inakadiriwa gharama ya kujitoa kutoka Jumuiya ya Ulaya ni kupunguza pato la taifa la Uingereza kwa asilimia sita ifikapo mwaka 2030 na kusababisha kila familia ipoteze wastani wa paundi 4300 sawa na Sh milioni 13.7 kila mwaka. Watu zaidi ya 400,000 wanaweza kupoteza ajira na thamani ya paundi itaporomoka.
Kura ya maoni haina nguvu za kisheria za kuiondoa Uingereza kutoka Jumuiya ya Ulaya. Mchakato wa kujitoa na kushauriana taratibu mpya za uhusiano kati ya Jumuiya ya Ulaya na Uingereza utaanza wakati Serikali ya Uingereza itakapoiarifu Jumuiya ya Ulaya kuwa itatumia kifungu cha 50 cha Mkataba wa Jumuiya ya Ulaya kujiondoa kwenye Jumuiya hiyo. Suala ngumu ni kujua serikali gani itakayokuwa madarakani ikiwa Waingereza wataamua kujiondoa Jumuiya ya Ulaya. David Cameron atalazimika au kulazimishwa na Wabunge wenzake wa chama cha Conservative kujiuzulu. Nani atakayechaguliwa kuongoza chama cha Conservative na kuwa Waziri Mkuu, ikiwa wanaotaka Uingereza ijiondoe kutoka Jumuiya ya Ulaya watashinda.
Je, Boris Johnson atachaguliwa na wabunge wa Chama cha Conservative kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza? Kampeni ya kura ya maoni imeongeza uhasama wa kisiasa ndani ya chama hicho. Inawezekana mgogoro wa kisiasa ukasababisha kuitishwa kwa Uchaguzi Mkuu.
Mgogoro wa kisiasa unaweza ukachukua muda na kusababisha hali ya wasiwasi kuhusu shughuli za biashara, fedha na uchumi.
Wasiwasi huo utahatarisha uchumi wa Uingereza kuporomoka na kuwepo mtikisiko wa uchumi wa nchi za Ulaya na duniani kote kwa sababu nchi za Jumuiya ya Ulaya zinazalisha karibu robo ya pato la dunia.
Ikiwa Uingereza itajitoa rasmi itabidi ifanye mashauriano na Jumuiya ya Ulaya ya taratibu za kufuata katika biashara na mahusiano ya kiuchumi kati yake na Jumuiya katika kipindi kisichozidi miaka miwili. Bila shaka Jumuiya ya Ulaya itaiwekea Uingereza masharti magumu ili nchi nyingine zilizomo ndani ya Jumuiya zisifanye uamuzi wa kujitoa. Uingereza inaweza kuwewekewa masharti yanayofanana na masharti iliyowekewa Norway na Uswissi. Nchi hizi si wanachama wa Jumuiya ya Ulaya. Raia wa nchi hizi mbili walikataa kujiunga na Jumuiya ya Ulaya katika kura ya maoni. Ili wafanye biashara huru na nchi za Jumuiya ya Ulaya inawalazimu kufuata sheria na taratibu za Jumiuiya hiyo.
Pia wanalipa mchango wa bajeti ya Jumuiya ya Ulaya pamoja na kwamba hawashiriki katika kuamua sheria na taratibu za kuendesha jumuiya hiyo. Uingereza haitafanikisha lengo la kujiamulia mambo yake yenyewe. Itafuata taratibu za Jumuiya ya Ulaya bila kushiriki katika kuziamua.
KUSAMBARATIKA KWA UINGEREZA
Ikiwa Waingereza watapiga kura kujitoa Jumuiya ya Ulaya, Uingereza yenyewe inaweza kusambaratika. Mwaka 2014, Scotland inayoongozwa na Chama cha Utaifa wa Scotland ilipiga kura ya maoni kuhusu kujitoa kutoka Muungano wa Ufalme (United Kingdom-UK). Waskoti wengi walipiga kura ya kubakia UK. Lakini asilimia 45 walitaka kujitoa.
Hata hivyo kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015,Chama cha Utaifa wa Scotland kinachounga mkono Scotland huru kilishinda kwa kupata wabunge 56 kati ya 59 wa Scotland.
Kura za maoni zinaonyesha Waskoti wengi wanapenda kubakia katika Jumuia ya Ulaya. Lakini kura za Waskoti ni chache, chini ya asilimia 10 ya kura zote za Uingereza. Ikiwa kura za Waskoti zitaamua kwa wingi kubakia katika Jumuiya ya Ulaya lakini kura nyingi za Uingereza yote zikaamua kujitoa, bila shaka waskoti watadai kura nyingine ya maoni ya kuwa na taifa huru la Uskoti ili wajiunge na Jumuiya ya Ulaya.
Ikiwa Uingereza itapiga kura kujitoa Jumuiya ya Ulaya, amani ya Ireland ya kaskazini ambayo kwa muda mrefu ilikuwa na machafuko ya kisiasa kati ya Wakatoliki na Waprotestanti inaweza kuathirika hasa kwa kuzingatia kuwa Ireland itaendelea kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Ulaya.
Itabidi kuwepo na usimamizi na udhibiti wa mpaka kati ya ya Ireland ya Kaskazini na Ireland ya Kusini. Wakatoliki wa Ireland ya Kaskazini wanapendelea kujiunga na Jamhuri ya Ireland wakati Waprotestant wanataka kubakia sehemu ya Uingereza.
Kujitoa Uingereza toka Jumuiya ya Ulaya kutaathiri nguvu za kisiasa na kidiplomasia za Jumuiya ya Ulaya. Uingereza ni nchi ya pili kwa ukubwa wa uchumi katika Jumuiya ya Ulaya baada ya Ujerumani. Uingereza ndiyo yenye jeshi kubwa kuliko nchi nyingine yeyote ya Jumuiya ya Ulaya. Uwezo wa jumuiya ya Ulaya kukabiliana na Urusi kidiplomasia utapungua.
KURA YA KUJITOA INAWEZA IKASHINDA?
David Cameron ndiye aliyeitisha kura ya maoni. Pamoja na kuthibitishwa na taasisi za kimataifa kuwa kuna athari kubwa za kiuchumi ikiwa Uingereza itajitoa kutoka Jumuiya ya Ulaya, wapiga kura wengi hawaamini taarifa hizo. Wanadhani kuwa ni propaganda ya wanaotaka Uingereza ibakie ndani ya Jumuiya ya Ulaya. Wanajiuliza kama kweli Cameron alijua kujitoa kuna gharama kubwa kwanini aliitisha kura ya maoni ya suala hili? Wanavutiwa na utaifa wa kiingereza.
Inawezekana kuwa wapiga kura wengi wa Uingereza wanataka nchi yao ibaki katika Jumuiya ya Ulaya. Hata hivyo wale wanaotaka ijitoe wamehamasika zaidi ya wale wanaotaka wabaki. Huenda wanaotaka kujitoa wakajitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na wale wanaotaka Uingereza ibaki katika Jumuiya wasiende kupiga kura kwa wingi. Bila kutarajia Uingereza inaweza kujitoa Jumuiya ya Ulaya na kusababisha mtikisiko mkubwa wa kiuchumi na kisiasa. Historia itamhukumu David Cameron kwa kusababisha vurumahi hiyo.
Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya uchumi, siasa na jamii.