Na LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM
MAKAMU wa Rais mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilal, amesema Afrika inapaswa kulipa uzito mkubwa tatizo la mabadiliko ya tabianchi kwa sababu suala hilo haliepukiki kutokana na bara hilo kukabiliwa na matatizo yatokanayo na mabadiliko hayo.
Dk. Bilal ambaye ni mtaalam wa nyukilia alisisitiza kuwa viongozi wa Afrika hawana budi kukabiliana na tatizo hilo kwa kuwa bara hilo liko chini kimaendeleo na upatikanaji wa huduma muhimu kama chakula, afya na elimu ya msingi bado ni changamoto.
Kauli hiyo aliitoa juzi jijini Dar es Salaam katika kongamano la kujadili mabadiliko ya tabianchi yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Dk Bilal alisema mabadiliko ya tabia nchi huathiri nyanja zote muhimu katika maisha kama mzunguko wa malisho unaotegemewa kwa maisha ya binadamu na viumbe hai kama vile maji na viumbe wa majini.