24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wapakistani waamuriwa kulipa faini milioni 126/-

koti1

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

RAIA watatu wa Pakistan, wamehukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 126 kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), baada ya kukiri kosa la kuingiza nchini vifaa vya mawasiliano na kuendesha biashara hiyo bila leseni.

Hukumu hiyo ilitolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.

Washtakiwa waliokiri kosa ni Hafees Irfan, Mirza Irfan Baig na Mirza Rizwani Baig na kukubali maelezo ya awali.

Hakimu Mwijage alisema kutokana na washtakiwa kukubali makosa kama walivyoshtakiwa na kukubali maelezo ya awali, mahakama hiyo inawaona wanahatia.

Kabla ya kutolewa adhabu, Wakili wa Serikali Mkuu, Johannes Kalungura akishirikiana na Wakili wa Serikali, Ester Martin, walidai washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza, hata hivyo wanaiomba mahakama itoe adhabu kali kwa kuwa makosa kama hayo yanahatarisha usalama wa nchi na  yanaisababishia hasara.

Alidai nchi ipo katika wimbi ambalo makosa kama hayo yanajirudia na Serikali ipo katika mkakati wa kukomesha ikiwezekana yasiendelee tena.

Kwa upande wa mawakili wa upande wa utetezi, Mohammed Majaliwa na Samwel Shadrack, walidai washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza wa kosa la kuendesha shughuli za mawasiliano bila ya leseni, hivyo wanastahili kupewa adhabu kulingana na kosa hilo.

Walidai washtakiwa hao wameona, wana watoto na wazazi wanaowategemea na wamekaa gerezani kama mahabusu kwa takriban miezi 13, ambayo ni adhabu tosha kwa makosa waliyofanya.

Baada ya kusikiliza hoja hizo Hakimu Mwijage alitoa adhabu ambapo alisema mahakama imezingatia maelezo ya pande zote mbili, hivyo inawaadhibu washtakiwa katika shtaka la kwanza kwa pamoja kama walivyoshtakiwa kulipa faini ya Sh milioni tano na wakishindwa watakwenda jela mwaka mmoja.

Katika mashtaka ya pili, tatu na nne,  Hakimu alisema washtakiwa hao kwa pamoja katika kila shtaka watalipa faini ya Sh milioni tano na wakishindwa watatumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela.

Aliamuru kwamba kila mshtakiwa atalipa Sh milioni 35 kama hasara  waliyoisababishia nchi hususan mamlaka husika (TCRA).

Upande wa Jamhuri uliwakumbusha washtakiwa hao mashtaka manne yanayowakabili, ambayo walikiri kuyatenda.

Akiwasomea maelezo ya awali ambayo washtakiwa waliyakubali, Ester alidai washtakiwa ni raia wa Pakistan ambao wana uhusiano wa karibu na kwamba tarehe isiyofahamika wakiwa Pakistan na watu wengine walikubaliana kutenda kosa Tanzania.

Washtakiwa walikubali kwamba kutokana na makubaliano hayo, watafuta na kununua vifaa ambavyo watavisimika kwa ajili ya mawasiliano ya kimataifa bila ya kutumia njia halali ya TCRA.

Hata hivyo walikubali ili kufikia malengo yao waliamua kusafiri kwenda nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania na waliingia tarehe tofauti na kwenda kuish katika hoteli ya Butterfly iliyoko Kariakoo, wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Washtakiwa hao walikubali katika hoteli hiyo walikuwa wakiishi katika chumba kimoja chenye namba 905, ambako walianza kuendesha shughuli hizo za mawasiliano bila ya kuwa na leseni ya TCRA.

Oktoba 5, mwaka jana, maofisa wa Polisi na wa TCRA wakati wakiendelea na uchunguzi walienda katika hoteli hiyo kwenye chumba cha washtakiwa na kuwakuta na vifaa mbalimbali vya mawasiliano.

Washtakiwa hao walikiri kukutwa na vifaa hivyo vikiwemo kadi za  simu za Airtel, kompyuta mpakato na kwamba waliisababishia TCRA hasara ya Sh milioni 140. 049.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles