25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

ATCL: Tunakuja na mapinduzi usafiri wa anga

ATCL 2

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

SHIRIKA la Ndege la Tanzania (ATCL), limesema ujio wa ndege zake mpya mbili aina ya Bombardier Q400 zinazotarajiwa kuwasili nchini Septemba mwaka huu, utaleta mapinduzi makubwa kwa huduma na utendaji ndani ya shirika hilo.

Pamoja na hali hiyo uongozi wa ATCL umetoa shukrani kwa Rais Dk. John Magufuli, kwa nia yake ya dhati ya kulifufua shirika hilo ambalo liliyumba kutokana na madeni ya ndani na nje.

Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Patrick Itule, alisema  ujio wa ndege hizo utalirejesha shirika hilo kwenye biashara ya ushindani dhidi ya makampuni mengine ya ndege nchini.

Ndege hizo zinazotengenezwa na kampuni ya Bombardier ya nchini Canada zinatarajiwa kuwasili nchini mwishgoni mwa Septemba mwaka huu.

“Baada ya ujio wa ndege hizi hatuoni tena sababu ya sisi kukwama na tutakuwa tumeingia rasmi kwenye biashara ya ushindani kwa kuwa changamoto kubwa ya uhaba wa ndege ambayo imekuwepo kwa miaka kadhaa sasa itakuwa imeanza kutatuliwa,’’ alisema Mhandisi Itule

Kaimu Mkurugenzi huyo wa ATCL, alisema shirika hilo halitakuwa tayari kuwavumilia wafanyakazi watakaoshindwa kuendana na kasi ya mabadiliko ya sasa.

“Tumejipanga kuboresha mfumo mzima wa utendaji kazi na hiyo ni  kuanzia mfumo wa ukataji tiketi na huduma zote muhimu kwa wateja ndio maana kwasasa tunawekeza zaidi kwenye  ubora wa rasilimali watu ili kuwavutia zaidi wateja…uvutiaji ambao utaambatana na utoaji huduma kwa gharama nafuu,’’ alisema

Akizungumzia uwezo wa ndege hizo, Ofisa Biashara wa Shirika hilo, Josephat Kagirwa, alisema zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na kwamba ujio wake utaongeza njia za kusafiri kwa shirika hilo kutoka njia mbili za sasa hadi kufikia njia zaidi ya kumi.

“Tutakuwa na madaraja mawili yaani daraja la uchumi litakalohusisha abiria 70 na daraja la biashara  litakalohusisha abiria sita kwa kila ndege. Kwa ujio wa ndege hizi tutaweza kuongeza safari za ndani na baadaye mwakani itakapopatikana ndege ya tatu kama Mheshimiwa Rais Magufuli,  alivyoahidi ndipo tutaanza safari za nje ya nchi tukianza na nchi jirani,’’ alisema

Alitaja baadhi ya mikoa ambayo shirika hilo litaboresha zaidi safari zake kuwa ni pamoja na Dodoma, Mwanza, Arusha, Mbeya, Kigoma, Tabora, Mpanda, Kilimanjaro, Mtwara, Zanzibar, Pemba, Bukoba  pamoja na Visiwa vya Comoro.

Hata hivyo alisema kwamba safari hizo katika maeneo tajwa na kwingineko zitaanzishwa baada ya kufanyika kwa upembuzi yakinifu.

“Lengo ni kuhakikisha tunakuwa tayari kutoa huduma nje ya nchi ndani ya muda mfupi iwezekanavyo ili tuweze kutimiza wajibu wetu kama shirika la ndege la taifa kwa kutangaza nembo ya taifa letu nje ya nchi, kusafirisha watanzania sambamba na kukuza utalii kwa kuwaingiza na kuwasambaza  watalii ndani na nje ya nchi kwa urahisi,’’ alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles