23.8 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Dunia ipo tayari kumpokea Semenya kwenye Olimpiki?

Caster Semenya
Caster Semenya

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

MWAKA 2009 ulizuka mjadala mkubwa duniani kuhusu kiwango cha homoni cha mwanariadha raia wa Afrika Kusini, Caster Semenya, ambaye anadaiwa kuwa na jinsia mbili na kuwa na tabia za kiume zaidi ya zile za kike, hali ambayo ilizua utata wa kisheria kuhusu namna ya kukabiliana na wanariadha wanawake wa haina hiyo.

Tukio hilo lilitokea wakati huo Semanya akiwa mshinda wa mbio za mita 800 katika mashindano ya dunia yaliyofanyika mwaka 2009 jiji la Berlin, Ujerumani.

Baadaye Semenya, ambaye alikuwa na umri wa miaka 18, alitakiwa kusimamisha zoezi la ukimbiaji baada ya kesi hiyo ya aibu iliyomwondoa kushiriki michuano hiyo hadi Julai mwaka 2010.

Matokeo ya kesi yake, Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF) na Kamati ya Olimpiki (IOC) yalikuja na sheria ya kwamba  kuwepo na  ukomo wa juu wa homoni kwa wanariadha wenye  jinsia mbili ambapo uamuzi huo utafanyika bila kuwa na haja  kufanya matibabu au hata upasuaji ili kuruhusiwa kushindana katika michuano hiyo.

Semenya anadaiwa kuwa na jinsia mbili huku mwili wake bado haujathibitisha moja kwa moja kwamba ni mwanamume au mwanamke.

Kiwango cha homoni kilichokutwa katika mwili wake ni kikubwa kuliko kilichpo kwa wanawake na kuibua maswali huenda akawa hana haki ya kuwa mwanamke kibiolojia.

“Watu wa aina hii hawatakiwi kukimbia na sisi,” ilisikika sauti ya mwanariadha wa mbio ndefu wa nchini Italia, Elisa Cusma mwaka 2009, baada ya Semenya kugundulika kama ana jinsia mbili.

Cusma anasema kwamba kutokana na vipimo hivyo, anamwona Semenya kuwa ni mwanamume na si mwanamke kama ambavyo wengine wanadai.

Hata hivyo, kwa miaka mingi IAAF na IOC, imekuwa ikihaha kutafuta suluhu ya jambo hili.

Tangu mwaka 2011 umakini katika jambo hili ulizidi kuongezeka kwa wanariadha aina ya Semenya ambao homoni zao za kiume ni nyingi zaidi ya kike, hivyo kuamuliwa kuondolewa katika mashindano makubwa kama vile Olimpiki.

Lakini kwa mara ya kwanza baada ya kupita zaidi ya miaka 50 katika michuano ya Olimpiki wanawake hawataondolewa kwa tatizo lolote la jinsia katika michuano ya Olimpiki inayoendelea jiji la Rio de Janeiro, Brazil.

Uamuzi huo utajumuisha pia wanariadha wenye jinsia mbili wenye viwango vikubwa vya homoni za kiume watachuana katika michuano hiyo.

Uamuzi huo unakuja kwa sababu ya  sheria ya IAAF kusimamishwa mwaka jana na Mahakama ya usuluhishi ya Michezo (CAS) iliyodai kwamba hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kwamba wanawake wenye viwango vikubwa vya homoni za kiume wanafaidika na hali hiyo katika riadha.

Mahakama hiyo iliwapa IAAF mwisho Julai 2017 ili kupeleka vithibitisho zaidi ya kama hali hiyo inaongeza ari au nguvu ya ziada kwa mhusika.

Kwa sasa wanasayansi bado wanahaha kutafuta ukweli kwamba hali hiyo inaweza kuathiri kiwango cha mhusika.

Hata hivyo, sheria hiyo iliwahi kukumbwa na changamoto katika Mahakama ya usuluhishi wa migogoro ya michezo mwaka jana kwa mwanariadha raia wa nchi ya India, Dutee Chand, kusimamishwa kushiriki  michuano mbalimbali ya riadha kwa miaka miwili kama ushahidi wa kipimo chake cha homoni hakitaendana na kinachohitajika ili kushiriki michuano hiyo.

Rais wa IAAF, Lord Coe, ambaye alikuwa akizungumza baada ya Mkutano wa wanamichezo kabla ya kuanza kwa michuano ya Olimpiki jijini Rio de Janeiro, Brazil, aliihoji Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo kama ni sawa kuendelea na sheria ya kiwango cha homoni au kipengele hicho kitupiliwe mbali.

“Sidhani kama tutakuwa tumevunja sheria kwa kufanya hivyo, kwa pamoja kama wanamichezo tulishangazwa na uamuzi wa sheria hiyo, nafikiri IOC ilifanya uamuzi mgumu kwa hili ambapo mabadiliko ni mawazo ya mashirikisho mengi.

“Tupo chini ya Mwenyekiti, (Mwenyekiti wa zamani wa Tume ya madawa ya  IOC) Arne Ljungqvist, ataangalia tena juu ya suala hili na kulirudisha Mahakamani ili kulifanyia marekebisha mwakani.

“Lakini tunatakiwa kukumbuka kwamba jambo hili ni la kibinadamu na lenye kuvuta hisia za wengi, ikizingatiwa ni wanariadha watoto wa kike na wakina dada,” anasema Coe.

Coe anasema kwamba jambo hilo litaangaliwa na Mahakama hiyo kwa kuwatumia watu sahihi ili kupatiwa ufumbuzi.

Wito huo wa Coe umekuja wiki moja kabla ya Semenya kuanza kampeni za ubingwa wa mbio za mita 800 jijini Rio, akiwa miongoni mwa wanariadha wanaotarajia kunyakua medali ya dhahabu katika mbio hizo.

Kiwango chake kimeshuka tangu mwaka 2009, lakini aliweza kunyakua medali ya fedha mwaka 2012 katika michuano iliyofanyika London akiwa nyuma ya Warusi ambao wamekuwa wakihusishwa na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu.

Msimu uliopita alipata taabu sana kurejea katika kiwango chake, lakini akiwa na miaka 25 kwa sasa anaonekana kuwa mwepesi  wa kukimbia mbio ndefu kuanzia mita 400 hadi mita 800.

Lakini kwa hisia za dhati na nguvu kwa pande zote za mjadala sasa zimethibitisha kwamba sheria hiyo iondolewe, kwani kwa sasa kama Semenya atafanikiwa akiwa Rio atakuwa kwenye hatari dhidi ya udhibiti wa sheria hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,719FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles