LNa Nora Damian, Mtanzania Digital
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limewatoa hofu Watanzania na kusema ndege zake ziko salama na hitilafu iliyotokea hivi karibuni ni ya kawaida.
Ndege ya Airbus A 220 – 300 ambayo ilikuwa ikielekea Mbeya ililazimika kujerea Dar es Salaam kutokana na hitilafu iliyotokea katika moja ya injini zake.
Akizungumza Februari 29,2024 na Waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Mhandisi Ladslaus Matindi, amesema hitilafu hiyo ilikuwa ndogo na ya kawaida.
“Injini moja ilipata joto na ikawa na mafuta mengi ndiyo yaliyosababisha moshi ambao uliingia kwenye mifumo ya hewa na kuwafikia abiria lakini si ndege kuungua moto kama ilivyoelezwa.
“Hali haikuwa ya kutisha na marubani na wahudumu walijitahidi kuchukua hatua za kiusalama kwa kuwapa taarifa abiria na kuwasihi wasiwe na wasiwasi,” amesema Matindi.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, hitilafu hiyo ilidumu kwa dakika tano kisha ndege ilirudi Dar es Salaam na abiria walibadilishiwa ndege nyingine na kuendelea na safari.
Naye Mkuu wa Usalama wa ATCL, Emmanuel Tivai, amesema hitilafu iliyotokea ni ya kawaida kwa vyombo vya usafiri na kwamba wahandisi wanaendelea kufanya uchunguzi.
Mmoja wa wahudumu aliyekuwepo katika ndege hiyo, Mwanaidi Mwanga, amesema mafunzo ya usalama waliyoyapata yaliwawezesha kudhibiti taharuki iliyokuwa imetokea.