MORONI,Comoro
RAIS Azali Assoumani ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Jumapili katika maeneo mbalimbali nchini humu.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyochapishwa juzi jioni na Tume ya Uchaguzi yamempa Rais Assoumani ushindi wa kishindo wa asilimia 66.77 ya kura.
Kwa ushindi huo, Rais Assoumani amemwacha mbali mpinzani aliyeshika nafasi ya pili, Mahamoudou Ahamada ambaye kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa ameambulia asilimia 14.62 ya kura zilizopigwa, na kwa maana hiyo haitahitajika duru ya pili.
Hata hivyo hata kabla ya matokeo hayo kutangazwa, tayari upinzani ulikuwa umekwisha kuyapinga ukidai kuwa upigaji kura uliandamwa na kasoro nyingi ambazo ziliripotiwa na tume ya uchaguzi.
Upinzani huo ulizilinganisha kasoro hizo na mapinduzi dhidi ya serikali, na kutoa wito kwa umma kusimama kidete na kuipinga hali hiyo.
Ahamada alikwenda mbali na kuitaka Jumuiya za Kimataifa kutoutambua ushindi wa Rais Assoumani
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Rais Assoumani amekiri hitilafu zilijitokeza.
”Ni kweli makosa yalifanyika, lakini tunafurahi kwa sababu hali ingeweza kuwa mbaya zaidi,” alisema Rais Assoumani na kuongeza kuwa wanajipongeza, na kumshukuru Mungu na Wakomoro.