Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Elisante ole Gabriel, amemteua Zamaradi Kawawa kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo).
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilisema hatua hiyo imetokana na aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene, kuhamishiwa Wizara ya Mambo Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, atakakopangiwa majukumu mengine.
Zamaradi alikuwa Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya uratibu wa mawasiliano serikalini wa wizara hiyo.
Assah Mwambene aliteuliwa Agosti, 2012 kuwa mkurugenzi wa idara hiyo na alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Clement Mshana ambaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Tanzania(TBC).
Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Ashukuru
Akizungumzia mabadiliko hayo, Mwambene alisema alipata fursa ambayo wengine hawakuipata kwa miaka minne.
“Namshukuru Mungu kwa nafasi hiyo na ninamshukuru Mheshimiwa Rais aliyeona kwamba naweza kumsaidia katika eneo hilo na kwa sasa niko tayari tena kwa furaha kutimiza wajibu wangu kwa nafasi nyingine.
“Nawashukuru nyote kwa ushirikiano mlionipatia nikiwa katika nafasi ya ukurugenzi. Nitaendelea kuwa mtumishi wa umma mwaminifu katika nafasi nitakayopewa kufanya.
“Mwisho nimepata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wakurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) akiwemo Raphael Hokororo, Jamal Zuberi, Vicent Tiganya na Zamaradi Kawawa.
“Nimejifunza mengi kwao pamoja na uongozi wa wizara. Nilianza kuonja utendaji kazi uliotukuka wa Mhe Nape Nnauye na Katibu Mkuu, Profesa Elisante ole Gabriel,” alisema Mwambene.
Yakukumbukwa kwa Assah
Septemba 27, 2013, Serikali kupitia Msajili wa Magazeti wa wakati huo, Assah Mwambene, ilitoa tangazo la kufungiwa kwa magazeti la ya MTANZANIA na Mwananchi.
Magazeti hayo yalifungiwa kwa kile kilichodaiwa ni mwenendo wa magazeti hayo kuandika habari na makala za uchochezi na uhasama kwa nia ya kusababisha wananchi wakose imani kwa vyombo vya dola hivyo kuhatarisha amani na mshikamano nchini.
Gazeti la MWANANCHI lilifungiwa kutochapishwa kwa siku 14 kuanzia 27 Septemba 2013.
Kwa upande wa gazeti la MTANZANIA, Mwambene alilifungia kutochapishwa kwa siku 90 kuanzia Septemba 27, 2013 kwa madai ya kuchapisha habari zenye uchochezi.
Julai 30,2012, Serikali ilitangaza kulifungia kwa muda usiojulikana gazeti la kila wiki la Mwanahalisi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kuandika habari na makala za uchochezi.
Mbali na hilo pia alisimamia kufungiwa kwa gazeti jingine la kila wiki la Mawio kwa kile kilichodaiwa kuandika habari za uchochezi kuhusu uchaguzi wa Zanzibar.