27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Askofu Kilaini: Kagera walazimishwe kulima

 RENATHA KIPAKA, Bukoba

ASKOFU Msaidizi Jimbo Katoliki la Bukoba mkoani Kagera, Dk. Methodius Kilaini, ameishauri Serikali ifanye kampeni ya kuwalazimisha wakazi wa mkoa huo kulima mazao mchanganyiko kukabiliana na tatizo la utapiamlo kwa watoto.

Pia aliitaka Serikali kuweka sheria kuanzia ngazi ya vijiji itakayombana kila mwananchi kuwa na shamba lenye mazao mchanganyiko tofauti na utamaduni uliozoeleka wa kutegemea kilimo cha migomba peke yake.

Katika mahojiano maalum na MTANZANIA juzi, Askofu Kilaini alisema Mkoa wa Kagera una uwezekano mkubwa wa kuzalisha chakula cha kutosha, lakini wakazi wake wamekuwa wavivu tofauti na mikoa mingine ambayo hali ya hewa ni ya ukame.

Alitolea mfano kwamba wanaume wa Mkoa wa Kagera wamekuwa wakitumiamuda mwingi kunywa pombe ijulikanayo kama ‘karandarugo’ – maarufu gongo nakuwaachia kazi ya kilimo wanawake ambao hata hivyo hawazalishi chakula cha kutosha kutokana na majukumu mengi waliyonayo.

“Kila mwananchi anatakiwa aulizwe shamba lake liko wapi na kama hana anatoa wapi chakula anachokula na familia yake. Ambaye hatakuwa na shamba basi achukuliwe hatua za sheria ili watu wote wawajibike katika kilimo.

“Endapo wanaume wa Mkoa wa Kagera watafanya kazi japo kwa saa tatu kila siku inavyotakiwa, familia zitapata chakula kingi na kilicho bora,”alisema Askofu Kilaini.

Alisema utamaduni wa wakazi wa mkoa huo unachangia tatizo la utapiamlo kwa kuwa asili yao ni kula ndizi na maharage tu.

Askofu Kilaini alisema bila kutungiwa sheria itakayowalazimisha kulima na kula vyakula vya aina nyingine, kiwango cha utapiamlo kitaendelea kuongezeka kila mwaka na kusababisha athari kubwa kwa jamii.

 “Wamezoea kula wali wakati wa sikukuu, kula ugali wakati wa maafa ya njaa na misiba, hivyo bila kampeni maalumu ya kuwabadilisha ni vigumu kutumia vyakula mchanganyiko kwa sababu si utamaduni wao,” alisema Askofu Kilaini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles