25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu Gwajima: Bila mshenga hakuna ndoa

gwajima askofuNa Asifiwe George, Dar es Salaam

ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, amesema tabia ya baadhi ya watu  kumuita  majina mengi ikiwa ni pamoja na ‘mshenga’, ni kielelezo dhairi kuwa sasa ni wakati wa mabadiliko na kwamba  bila mshenga   ndoa haiwezi kuwapo.

Askofu Gwajima aliyasema hayo jana kwenye Ibada iliyofanyika kwenye kanisa la Ufufuo na uzima lililopo Ubungo.

Matamshi hayo ameyatoa  ikiwa  imepita takribani wiki moja  tangu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa aseme kwamba kiongozi huyo wa dini ndiye mshenga aliyemkutanisha Mgombea Urais wa Ukawa, Edward Lowassa na yeye.

“Lakini niwaeleze kuwa hakuna mtu ambaye ananiweza mimi Gwajima  ndiyo mana hivi sasa wanahaha kwa kuniita majina mengi;  mara Mshenga, mara nani… lakini ieleweke kuwa hii ni saa yetu ya mabadiliko ambayo Mungu anataka kutupatia taarifa.

“ Wakati nakuja kanisani nilipofika hapa maeneo ya Ubungo kwenye stendi za daladala watu waliibuka na kuanza kupiga kelele wakiniita mshenga… mshenga….

“Sasa hii ni ishara tosha, maana ndoa bila mshenga haiwezi kuwa ndoa  na mshenga ndiye mwenye jukumu la kuunganisha kuwa kitu kimoja, na ikitokea kuna ugomvi  anao uwezo wa  kusuluhisha na kuweka mambo sawa,” alisema Gwajima.

Awali akianza mahubiri yake, Askofu Gwajima alisema anatambua kanisani hapo walikuwapo waandishi wa habari waliokuwa wanaosubiri atoe kauli ya kumjibu Dk Slaa, lakini hatofanya hivyo kwa kuwa kanisa ni sehemu ya kuhubiri Neno la Mungu na siyo uwanja wa siasa.

Kwa sababu  hiyo alisema atazungumza kila kitu kesho kwenye Hoteli ya Landmark  mkutano ambao utarushwa moja kwa moja na televisheni.

“Najua hapa kuna waandishi wa habari wamekuja, wanataka kujua jinsi nilivyokuwa mshenga, lakini kanisa langu siyo sehemu ya majibizano, nitafanya mkutano  Jumamne kwa saa moja.

“Muda huo unatosha kabisa kufafanua jinsi nilivyokuwa mshenga na  matangazo hayo yatarushwa moja kwa moja katika televisheni zote kuanzia saa 7:00 mchana hadi saa 8:00, hivyo msiwe na wasiwasi.

Alisema katika maisha yake hajawahi kuona mchungaji akiongoza nchi bali anachotambua kazi yake ni kuhubiri injili na kuwapatia waumini mafundisho  mema.

Askofu Gwajima alisema mwanzoni  mwa Januari mwaka huu kanisa hilo lilifunga siku 30 kwa ajili ya kutafuta kiongozi wa kuongoza nchi hivyo kiongozi atakayeapishwa mwaka huu atakuwa nao kwa sababu kanisa lilifunga na kuomba kwa ajili yake.

Alisema baadhi ya viongozi kusimama mbele ya vyombo vya habari na kusema   kuna mgombea urais ambaye ameletwa na Gwajima ni ishara nzuri.

“ Hivi mlishawahi kuona mtu anasimama kabisa kwenye vyombo vya habari na kusema mambo haya, ukiona dalili kama hizi ujue ndiyo tayari wamesha kwisha,” alisema.

Alisema wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu   Nyerere, wahubiri wakubwa wa Injili walikuwa ni Askofu Imanuel Lazaro na Dk. Moses Kulola.

“Mmoja alikuwa wa Tanzania Bara na mwingine Zanzibar, walikuwa wakihubiri injili , Nyerere baada ya kuona watu wanahamasika sana na  mahubiri yao na kumiminika kwenye mikutano yao, alisema huenda wangeleta mapinduzi ya siasa hivyo aliona ni bora kuwasambaratisha.

“Pamoja na kuwasambaratisha lakini kila mmoja alikwenda kuhubiri anapopajua na watu waliendelea kuhamasika, sasa wakati huu ni wa Gwajima kuwa mshenga, ukiona muumbaji ameonekana ujue lazima waliopo watapotea, hii ni saa ya ufufuo na uzima.

“Namuona Roho Mtakatifu awatembelee Lowassa (Edward Lowassa, Mgombea Urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)  na Magufuli (John Magufuli Mgombea urais wa (CCM), na atakayeshindwa akae pembeni lakini kanisa la ufufuo na uzima litabaki palepele”.

“Kwa sasa kila mtu apeleke bidhaa zake sokoni na kuzinadi kwa kuwa walaji wapo, walaji hao waamue wenyewe kuchagua bidhaa itakayomfaa kwa lengo la kupata kiongozi atakayeweza kusimamia misingi yote ya dini bila ubaguzi wowote. Muisilamu ahubiri kwa dini yake, Mkristo naye ahubiri kwa dini yake lakini siyo kiongozi mbaguzi,” alisema.

Baada ya kutoa kauli hiyo  aliendelea na mahubiri na katikati yake akasema, ‘lakini niwaeleze kitu, si mnakumbuka yule mtoto aliyekuja kupiga magoti hapa mbele ya madhabahu ya kanisa hili Januari mosi mwaka huu, sasa yule ni msaliti,” alisema na kanisa likashangalia huku waumini wakipiga kelele za ‘sema babaaaaa’, ‘ msaliti mkubwa huyoo’ .

Katika kanisa hilo waumini walionekana kuvaa nguo na vitambulisho vilivyokuwa na picha ya Mgombea Urais wa Ukawa, Edward Lowassa, huku vingine vikiuzwa katika kanisa hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles