22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa watumia kauli za Kinana kuichongea CCM kwa wananchi

MnyaaNa Elias Msuya, Tanga

ZIARA ya Mgombea Mwenza wa Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Juma Duni Haji, imeingia mkoani Tanga huku viongozi walio kwenye msafara wake wakiwakaanga wagombea ubunge wa CCM kwa kauli ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana aliyesema chama chake kimejaa wezi, wanafiki na majambazi.

Kinana alitamka maneno hayo alipozungumza kwenye mkutano wa hadhara  mjini Moshi mkoani Kilimanjaro juzi.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika wilayani Muheza jana, aliyekuwa Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa  alisema:

“Namhurumia sana huyu mtu aliyekuwa Balozi Zimbabwe (Mgombea Ubunge wa CCM jimbo la Muheza, Balozi Adadi Rajabu) kwa kuja kugombea ubunge kupitia chama hiki ambacho Katibu wake amesema kina wezi, majambazi na wanafiki. Namhurumia kwa sababu chama hiki hakitapita mwaka huu”.

Kuhusu kashfa ya Richmon, Mnyaa alisema: “Watu wanazungumzia Richmond, mimi nilikuwa mjumbe wa kamati ya Dk. Mwakyembe (Harison). Tulisema katika ukurasa wa 39 kwamba kuhusika kwa Lowassa ni kutokana na nafasi ya Waziri Mkuu kwa sababu ndiye aliyesimamia Serikali. Lakini hakuna mahali anapohusishwa moja kwa moja.
“Mbona hawazungumzii IPTL, mbona hawazungumzii Mgodi wa Kiwira?”

Akizungumza katika mkutano huo, mgombea mwenza wa Ukawa, Juma Duni, alisema umoja huo utatekeleza ahadi zilizoshindikana katika utawala wa CCM.
“Rais (Jakaya) Kikwete alisema atajenga kiwanda cha kukamulia maji ya matunda hapa Muheza na alisema ataubadlisha mji wa Tanga kuwa mji wa viwanda, lakini hakuna kilichofanyika, wameviua vyote. Sisi tutakapoingia madarakani hatutaahidi  ila tutatekeleza tu,” alisema Duni.
Kuhusu afya, alisema kutokana na uzoefu wake wa kuwa waziri wa afya wa Zanzibar atapigania afya hasa ya wanawake kutokana na umuhimu wao katika jamii.

“Mimi nimekuwa Waziri wa Afya kwa miaka minne na waziri wa miundombinu kabla sijastaafu. Najua kero za barabara zinazowakabili wananchi. Nazijua pia kero za afya…Siku hizi wanawake wanadhalilika wanapokwenda kuzaa,” alisema.

Kuhusu kero ya shamba la Ikunguru lililomo wilayani humo, Duni alisema atatatua kero ya wananchi waliowekwa kizuizini kwa kudai shamba hilo.

“Mimi mwenyewe nimefungwa jela miaka mine bila makosa na sijalipwa chochote. Tutamwagiza mbunge wetu ashughulikie kesi hiyo. Tunajua kero ya umasikini. Lowassa amesema anachukia umasikini na mimi pia. Tutapambana nao,” alisema.

Kuhusu elimu alisema Ukawa ikiingia  madarakani itatoa huduma hiyo bure kwa sababu vyanzo vya fedha vipo.
Alisema wakati watu wanalipishwa ada za shule, Serikali inatumia fedha nyingi katika sherehe na sikukuu zisizo na faida kwa wananchi.

“Jana nimesoma gazeti moja linahoji tutapata wapi fedha. Nikajiuliza hivi tuna sikukuu ngapi zinazogharimu fedha? Mapinduzi, kuzaliwa kwa CCM, Muungano, Sabasaba na nyinginezo… fedha nyingi zinazotumiwa. Tunazo rasilimali nyingi, madini, misitu, ardhi na vyanzo vya maji,”  alisema.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Muheza, Mathias  Kaluasha, alitaja kero zinazoikabili wilaya hiyo kuwa ni pamoja na maji.

“Maji yameshafika Kijiji cha Mlingano lakini Muheza hatuna maji. Hapa tuna mito miwili ni kama Euphrates na Tigris lakini tuna maji,” alisema Kaluasha.

Aliitaja Tarafa ya Amani wilayani humo kuwa ndiyo yenye uchumi wa wilaya hiyo kwa asilimia 50 lakini barabara yake haijawahi kujengwa kwa lami.

“Tunaomba Lowassa akija Muheza aende Amani, Dk. Magufuli anakuja Muheza na atakwenda Amani.

“Matatizo ya Muheza karibu yanafanana na mkoa mzima wa Tanga. CCM imefanya hayo kwa makusudi ili Watanzania waendelee kukiabudu,” alisema.

Ukawa wamemsimamisha Ernest Msingwa wa Chadema kuwa mgombea ubunge  Muheza na katika Wilaya ya Pangani wamemsimamisha Amina Mwidau wa CUF.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles