Na Mwandishi Wetu
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya, Evaristo Chengula amesema maaskofu waliotoa waraka kama ujumbe wa Pasaka hawana ubaya na mtu yeyote.
Amesema ujumbe ule wameutoa kwa kujihangaisha wote ili waanze kujiandaa kwa mwaka ujao wa uchaguzi, watu waweze kuchagua kiongozi bila kukosea.
“Tunaweza tukakosea lakini kwa vyovyote vile hatutapitia udhaifu wa watu wengine,” amesema Askofu huyo leo Ijumaa Machi 30, katika Ibada ya Ijumaa Kuu katika Kanisa la Bikira Maria wa Fatima, Parokia ya Mtakatifu Francisco wa Asizi Mwanjelwa, Jimbo Kuu la Mbeya.
Pamoja na mambo mengine, Askofu Chengula amesema anajua kwamba watu wanamchagua mtu wa aina gani, lakini hawawaambii sasa ni wakati wa kuchagua chama fulani kwa lazima.
“Je, tukiwapatia mtu fulani ambaye haendani na matakwa yao, itakuwaje? Tunakuwa hatujatenda haki. Kila parokia ikae na mapadre wao waongee, watathmini na waumini wao kama yupo mtu, ili tuweze hata sisi kutimiza azimio la Umoja wa Mataifa waliofanya miaka 70 iliyopita kwamba kila mmoja lazima aishi akitendewa haki na mwisho kuwe na amani.
“Kila mara baada ya uchaguzi tumekuwa tukikimbizana kama sungura na mbwa hii maana yake nini, maana yake tunachagua mtu ambaye hawezi kutusaidia, badala ya kufikiri kwamba yule aliyechagualiwa atufanye tupate haki zetu na sisi tuishi kwa amani,” amesema Askofu Chengula.
Aidha, Askofu Chengula amesema, waliwachagua viongozi hao lakini wanaishi katika hali ya woga woga.
“Mwaka 2019 tuchague watu ambao si wabinafsi, tunaweza tukakosea lakini tutajitahidi kwa vyovyote vile hatutapitia makosa ya watu wengine kwa sababu tukipata viongozi wabaya ni makosa yetu wote, hawa waliopo hawakujiweka wenyewe ni mimi na wewe tumewaweka, tuwe pamoja nao katika sala katika kutimiza mazuri waliyoweka ili watakaokuja wawe na uwezo wa kuyaendeleza na tutakaowachagua wasiwe na roho za ubinafsi.
“Kila mmoja aende kasimulia huko anakokwenda kwa sababu ni vita ya wote, tukipata viongozi wabaya au wazuri, kila mmoja ana haki ya kuona Tanzania ina upendo na mshikamano baina yetu wote,” amesema.