ELIYA MBONEA, ARUSHA
ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mount Kilimanjaro (DMK), Dk. Stanley Hotay, ameyataka mataifa ya nje kushughulika na mambo yao, kutoa ushauri na si kuiamulia Tanzania ifanye nini.
Kauli hiyo aliitoa jijini hapa jana katika uzinduzi wa mpango mkakati wa kuboresha elimu mkoani Arusha, uliozinduliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Suleiman Jafo.
Akitoa salamu kwa wadau wa elimu waliohudhuria uzinduzi huo, Askofu Dk. Hotay alimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa usimamizi wa jumla wa nchi na Serikali japokuwa kumekuwapo kelele nyingi kutoka kwa mataifa ya nje yakitaka kuingilia.
“Kama utapangiwa namna ya kuishi na jirani yako basi huna maisha, akikupangia jema leo, kesho mabaya yatakuja.
“Katika hili tunampongeza sana Rais Dk. Magufuli kwa kusimama imara, kwamba mataifa ya nje na nchi hii yashughulike na mambo yao, kwetu washauri lakini si kutuamuria,” alisema Askofu Dk. Hotay.
Kuhusu elimu, alisema ni ukombozi na kwa Wakristo wanaamini hivyo na hata kwa wasio Wakristo.
“Mtihani uliopita umetutia moyo kwa maana ya kwamba sasa si kukariri tu bali mitihani itawafanya vijana kufikiri, mitihani mingi nyuma uliweza kugusa kwa kidole katika karatasi ya mtihani na ukafaulu na kufeli.
“Mitihani ya sasa ambayo kuchagua si kwa wingi itafanya vijana kufikiri, itawasaidia kwa ujumla, tuwatakie heri ya Krismasi na mwaka mpya ujao, katika juhudi sisi viongozi wa dini tutasimama nanyi, wajibu wa kazi yetu kwanza ni kuwaombea.
“Lakini mnapozalisha kwa wingi walimu na watumishi muangalie soko na mahali pa kuwapeleka ili vilio vikapungue mitaani, wakimaliza mbio hawajui pa kwenda, maumivu yanaongezeka badala ya kupungua.
“Ama namna ya ufundishaji ibadilike, kwamba wajue kujitegemea katika maisha haya na wasitazamie ajira ambayo haipatikani au wanabaki kusubiri.
“Waziri ombi letu kwenu mkalisimamie na kutusaidia kupunguza vijana wengi wenye shahada za kutosha na taaluma mbalimbali wapate ajira,” alisema Askofu Dk. Hotay.
Kwa upande wake, Jafo alimpongeza Mkuu wa Mkoa, Mrisho Gambo na wasaidizi wake kwa kubuni jambo muhimu linalolenga kutekeleza ndoto za Rais.
Alisema Arusha imeweza kufanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba kwa kushika nafasi ya tatu kitaifa na aliwataka kuongeza juhudi za kuzalisha wanafunzi wenye uwezo ili washike nafasi ya kwanza kitaifa.
“Mkakati huu ni ajenda ya kumkomboa mtoto masikini anayetengewa na Serikali kiasi cha shilingi bilioni 23.5 kila mwezi kwa ajili ya elimu bila malipo chini ya Rais Dk. Magufuli.
“Jambo hili likisimamiwa vizuri Arusha itaiacha mikoa mingine kwa ufaulu na nawaomba wakuu wa mikoa wengine kuiga mfano huu katika kuboresha sekta ya elimu nchini,” alisema.
Naye Gambo alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutojisifu kuwa mkoa wake wa kwanza kwa sababu tayari ulihusika na masuala ya udanganyifu hivyo kupoteza sifa ya uaminifu.
“Dar es Salaam imekuwa ya kwanza, lakini wana madoa ya watu waliokutwa na kashfa ya wizi wa mitihani, mshindi wa pili alikuwa na tuhuma hizo. Arusha ni ya tatu haina tuhuma zozote, Makonda ni rafiki yangu naomba salamu hizi azipate aliko,” alisema Gambo.
Kuhusu mpango huo, alisema umewezesha kutatua changamoto ya ufaulu wa mitihani ikiwamo walimu kutofundisha mada zote au kutunga mitihani kulingana na silabasi walizofundisha.
“Tulifanya utafiti wa mtihani wa nusu muhula kidato cha kwanza hadi cha tatu, hakuna halmashauri iliyofikia asilimia 50, sayansi ilikuwa na wastani wa asilimia 30 na fizikia asilimia 44.
“Somo la hisabati kidato cha kwanza ilikuwa asilimia 20, kidato cha pili asilimia 13 na kidato cha kwanza asilimia 10. Baada ya matokeo hayo tayari tulijua mahali pa kuanzia mpango huu wa kuboresha elimu kwa mkoani kwetu.
“Mchakato huu ulianza mwaka 2017 ukishirikisha wadau mbalimbali ikiwamo wafanyabiashara waliowezesha kununua mashine za kuchapia mitihani ya majaribio kwa mkoa mzima kwa gharama nafuu ya shilingi milioni saba kwa mashine 10 badala ya shilingu milioni 20,” alisema Gambo.