NA RUTH MNKENI
MLEZI wa Chama cha Waimbaji wa Muziki wa Injili Tanzania (Chamwita), askofu, Rejoyce Ndalimo, amewataka waimbaji wa Injili wafanye biashara nyingine za kuwaingizia kipato huku wakiendelea na muziki.
Mbali na hilo amewataka waimbaji hao waache utamaduni wa kudurufu kazi za wenzao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Ndalimo alisema wokovu hautaki watu wajinga unataka watu wanaojibidisha na wanaotumia fursa zilizopo kujiongezea kipato cha kukuza uchumi wao.
“Kuokoka si kuwa mjinga, fursa za biashara zipo fanya ili uweze kujikwamua kiuchumi, pia mjiunge na bima ya afya ili kupunguza gharama za kumchangia mtu atakapoumwa badala yake tusaidiane wakati wa sherehe na mengineyo,” alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa, Joyce Hagu, alisema Serikali ipo katika mchakato wa kuanzisha mfuko wa wasanii kutokana na kutambua mchango wao katika jamii.