22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu amwangukia Magufuli

Pg 1>> Amtaka asiwatumbue misamaha ya kodi

>> Viongozi wa dini wasisitiza upendo, umoja katika familia

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

ASKOFU wa Kanisa la Anglikani nchini (KAT), Dayosisi ya Mount Kilimanjaro (DMK), Askofu Stanley Hotay, amesema kanisa halina majipu ya kutumbuliwa kwa kuwa linatoa huduma zinazoisaidia Serikali kupeleka maendeleo kwa Watanzania.

Kauli ya Askofu Hotay aliyoitoa mjini hapa jana wakati wa Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid imekuja wakati mwenendo wa uongozi wa Rais John Magufuli ni wa kutumbua majipu kutokana na kile alichokisema Februari, mwaka huu wakati akizungumza na wazee wa Dar es Salaam kuwa alikuta uozo mkubwa serikalini.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha mgeni rasmi katika ibada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daud Ntibenda, Askofu Hotay alipongeza juhudi na kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Magufuli.

Askofu Hotay ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Kanisa la Arusha alisema kumekuwapo na taarifa
za waraka wa kuondolewa kwa misamaha ya kodi kwa kanisa hatua aliyosema kama itatekelezwa itarudisha nyuma
juhudi za kuisaidia Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.

“Tunakuomba mkuu wa mkoa utusaidie kufikisha hili. Lakini pia liangaliwe vizuri sisi hatuna majipu kabisa.
Tunasaidiana na Serikali katika kutoa huduma za kijamii,” alisema Askofu Hotay.

Kwa upande wake, Ntibenda, aliwaomba viongozi wa kanisa kuisaidia Serikali kuhamasisha vijana kufanya
kazi.
“Rais Magufuli amenipa majukumu ya kuhakikisha watu wanafanya kazi hasa vijana badala ya kucheza mchezo wa pool.

Tabia hii ikiachwa itatengeneza Taifa la wavivu na walalamikaji,” alisema Ntibenda.
Alisema Serikali itaendeleza ushirikiano uliopo baina yake na taasisi za dini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watu
wake wanaendelea kuabudu kwa amani na utulivu.

Katika ibada hiyo, Ntibenda, alilazimika kutoa namba yake ya simu ambayo ni 0766030000 na 0754604003
baada ya kuwataka wananchi wasikubali kutoa rushwa katika maeneo ya huduma za kijamii.

“Nawaomba wananchi nipigieni simu pindi mnapoombwa rushwa katika huduma za kijamii na maeneo mengine.
Nisaidieni kupambana na vita hii,” alisema Ntibenda ambaye namba yake ilisomwa kwa wananchi na Askofu Hotay.

MAGUFULI

Kwa upande wake, Rais Magufuli, aliwashangaza waumini wa Kanisa la Mtakatifu Petro lililoko Oysterbay jijini Dar  es salaam baada ya kusimamisha msafara wake na kisha kusalimiana na walemavu.

Tukio hilo lilitokea jana katika lango la kutokea kanisani hapo ambako alikwenda kuhudhuria Ibada ya Ijumaa
Kuu.
Magufuli alifika kanisani hapo mapema na kusali pamoja na waumini wa kanisa hilo na ibada ilipoisha alipanda katika gari lake na kuondoka.

Wakati akiondoka alikuwa akiwapungia mkono waumini hao na alipofika langoni hapo ghafla msafara wake ulisimama na kisha kushuka ili kuwasalimia waumini hao jambo lililowafanya wengine kusogea
ili kujua kilichotokea.

Magufuli alishuka na kuwafuata walemavu waliokuwa wamekaa jirani na lango hilo la kutokea na kuzungumza
nao.
Ingawa mazungumzo hayo hayakusikika, kitendo cha kushuka na kuzungumza na walemavu hao kiliwafanya watu waliokuwapo jirani na eneo hilo kuvutiwa na alipomaliza alipanda tena katika gari yake na msafara huo kuondoka kuelekea Ikulu.

Awali, akizungumza katika mahubiri hayo, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro, Stephano Kaombwe, aliwasihi
Watanzania kuwa na moyo wa upendo.

Huku akinukuu katika Biblia Takatifu katika injili ya Yohana, Kaombwe alisema inashangaza kwamba Mungu
aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanaye wa pekee Yesu Kristo kwa ajili ya wanadamu lakini wenyewe bado
wanachukiana.

“Wanadamu hatukuumbwa tuteseke, ukisoma katika kitabu cha Mwanzo utaona Mungu aliwaweka Adam na
Hawa kwenye bustani ili waishi vizuri, wastarehe lakini walitenda uasi,” alisema Kaombwe.

LOWASSA

Kwa upande wake, aliyekuwa mgombea urais wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyeshiriki ibada hiyo katika Kanisa la Azania Front Kanisa aliwatakia
Watanzania washerehekee Sikukuu ya Pasaka kwa amani lakini alikataa kuzungumzia ya Zanzibar.

“Suala la uchaguzi wa Zanzibar siwezi kulizungumzia kwa sasa labda hapo baadaye lakini kufanyika kwa uchaguzi
huo ninamtukuza Mungu,” alisema Lowassa baada ya ibada hiyo kumalizika.

Awali akizungumza katika ibada hiyo, Mchugaji wa Usharika wa Azania Front, Charles Mzinga, alisema ni vyema wazazi watekeleze wajibu wao katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora.

“Watoto wetu tunapaswa kuwalea katika maadili yanayompendeza Mungu,” alisema mchungaji huyo.

Alisema kila mtu anapaswa kuwajibika ipasavyo ili kuhakikisha kila analolifanya linamtukuza Mungu ikiwa kazini
au katika jamii.
Wakati huohuo, katika mahubiri yake aliyoyatoa Kanisa Kuu Katoliki la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padre Nicholas Masamba, aliwataka Wakristo kuwajibika kutekeleza majukumu yao katika familia zao
na si kuwachia walimu peke yao.

“Tafakari hii ya kifo cha Yesu kusema yametimia, inarudisha swali kwetu ikitutaka tujiulize kuwa ni mangapi tumeyatimiza na sisi kwenye ngazi mbalimbali ikiwamo kazini, malezi ya familia na kwenye nafasi mbalimbali kama Wakristo,” alisema Padri Masamba.

Katika ibaada hiyo iliyohudhuriwa na waumini wengi akiwamo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema Wakristo wengi wamekuwa wakishindwa kutimiza majukumu yao katika
nafasi mbalimbali.

Habari hii imeandikwa na Faraja Masinde, Ruth Mnkeni na Veronica Romwald (Dar es Salaam) na Eliya Mbonea (Arusha)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles