23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu akemea viongozi jeuri

UPENDO MOSHA -MOSHI

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, amewataka viongozi wa ngazi za juu wa Serikali na wale wadogo kuacha tabia ya kukandamiza haki za wanyonge na kiburi cha madaraka.

Dk. Shoo pia aliwataka viongozi hao kuacha tabia ya majivuno, kujiinua na kiburi na kutumia unyonge wa wananchi masikini kutembea juu ya migongo yao.

Alitoa onyo hilo wakati akiendesha ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Dk. Reginald Mengi, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Usharika wa Moshi Mjini.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Dk. Shoo alisema baadhi ya viongozi hasa vijana, wamekuwa wakitumia madaraka na vyeo vyao kuwakandamiza wananchi wa chini kwa kuwanyima haki zao jambo ambalo halimpendezi Mungu.

“Baadhi yenu ninyi viongozi mmekuwa na kiburi na tabia ya majivuno na kujiinua na kukandamiza haki za wanyonge, nasema muache tabia hiyo.

“Viongozi wenye umri mdogo muache kujitutumua kama mabeberu, tuwe kama Dk. Mengi, licha ya uwezo wake alikuwa akijishusha na kuwasaidia wote, kila siku nasali kwa ajili ya viongozi, msipojishusha Mungu atawashusha, acheni.

“Hawa viongozi wadogo naona wanajitutumua kama chatu, acheni bwana atawashusha.

“Umepata kacheo kidogo, kaudiwani, ukuu wa wilaya, ukuu wa mkoa, uwaziri alafu unawaona wenzako sio kitu, acha mara moja.

“Kipimo mnachotumia kuwapimia wengine ndicho Mungu atakachotumia kuwahukumu, mmekuwa na kiburi cha madaraka na vyeo vyenu, lakini mkumbuke mwisho wa yote kuna kifo na hukumu juu ya matendo yenu,” alisema Dk. Shoo.

Alisema viongozi wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha wanatubu dhambi ya majivuno na kwamba wajibu wa viongozi ni kusimamia haki.

“Viongozi mmekuwa mkijivuna na kujifutua kwa sababu ya madaraka, mmesahau wajibu wenu, mmekuwa mkijifutua kama kifutu, vyeo hivi amewapa Mungu, mnapaswa kuwatendea wananchi haki na sio kuuza haki yao.

“Mmekuwa mkiwaonea watu wadogo, tumieni akili katika kutatua mambo,” alisema.

Aidha alisema kila Mtanzania ana wajibu wa kusimamia kweli kwani baadhi ya watu wamekuwa wakiupotosha ukweli ambao umekuwa ukionekana hasa katika masuala ya msingi.

“Kaeni na msimamie ukweli, kwa kufanya hivyo kwa pamoja tutasonga mbele, acheni ubinafsi na kujitutumua, simamieni ukweli,” alisema.

Mbali na hilo, Dk. Shoo aliwaonya baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakifanya mambo yenye ubaguzi jambo ambalo alidai limekuwa likiwagawa Watanzania.

“Tanzania katika dhambi ambayo inatutafuna ni ya ubaguzi, tunapaswa kutubu.

“Baadhi ya viongozi wamekuwa wakifanya mambo hayo ambayo Mbowe (Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe) pia aliyagusia, nasema acheni mara moja kama tunataka baraka,” alisema.

Awali Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, alikemea kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambaye wakati wa kuaga mwili wa Mengi jijini Dar es Salaam, alielezea sifa za marehemu akionesha kushangazwa na jinsi alivyoweza kusaidia masikini na hasa walemevu licha ya kwamba alikuwa Mchaga.

Akizungumzia suala hilo, Dk. Shoo alisema viongozi waache masuala ya kufarakanisha jamii na badala yake watumie uwezo wao wa uongozi kuiunganisha jamii.

ALITAKA BUNGE KUTENDA HAKI

Katika mahubiri yake, pia alitumia nafasi hiyo kumtaka Spika wa Bunge, Job Ndugai kutenda haki na kufanya maamuzi ambayo yana masilahi kwa wananchi wanaowawakilisha bungeni.

“Ndugai leo upo hapa, nasema mnapokaa bungeni na kuamua mambo, mtende haki na mfanye maamuzi yenye masilahi kwa wananchi,” alisema.

YA KWENYE MITANDAO

Dk. Shoo pia alionesha kusikitishwa na vitendo vya upotoshaji vinavyoendelea katika mitandao ya kijamii akiitaka familia ya Mengi kupuuza yote na watu hao kuacha mara moja tabia hiyo.

“Nasikitishwa na mambo yanayoendelea katika mitandao ya kijamii, naomba familia myapuuze yote na katika kipindi hiki kigumu mumuite Mungu awasaidie,” alisema.

AMZUNGUMZIA MENGI

 Akimzungumzia marehemu Dk. Mengi, alisema licha ya kuwa tajiri alikuwa mtu ambaye alitoa katika jamii na hakujikweza wala kuwa na kiburi jambo ambalo viongozi wanapaswa kuliiga.

“Mengi pamoja na kuwa na mapungufu yake kama binadamu, alikuwa mtu aliyejinyenyekeza katika jamii, naomba viongozi tuyaishi yale yote mazuri aliyoyafanya Mengi hapa duniani,” alisema.

Hata hivyo Dk. Shoo aliitaka familia kuwa wavumilivu katika kipindi hiki na kwamba Mengi amekwishamaliza kazi yake hapa duniani na wote wana wajibu wa kuyaenzi yale yote mazuri aliyoyafanya.

“Naomba familia mumshirikishe Mungu katika kila jambo, najua mpo katika wakati mgumu, kwamba Mengi kaacha watoto wadogo, naamini Mungu atawakuza, lakini muwalee katika maadili mema na kumjua Mungu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles