Derick Milton, Simiyu
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Simiyu imewafikisha mahakamani askari wa wanyapori 16 wa Hifadhi ya Akiba ya Maswa (Maswa Game Reserve) kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wafugaji zaidi ya milioni 70.
Askari hao wamo pia, kutoka kikosi dhidi ya ujangili (KDU) kituo cha Bunda mkoani Mara na watumishi watatu wa Kampuni ya Uwindaji ya Fredikin Conservation Fundi (FCF).
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake leo Kamanda wa Takukuru Mkoa, Joshua Msuya amesema kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kuomba na kupokea rushwa kwa nyakati tofauti ambapo kila mmoja anadaiwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh. 30,000 na 70,000.
Kamanda Msuya amesema watuhumiwa wote 19 wanakabiliwa na kesi za jinai kwa makosa ya kujihusisha na vitendo vya rushwa kinyume na kifungu cha 15 (1)(a) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Msuya amesema kuwa watuhumiwa hao kati ya April Mosi mwaka huu hadi Juni 30 mwaka huu wakiwa kwenye eneo lao la kazi Pori la akiba la Maswa upande wa Wilaya ya Itilima mkoani hapa kwa siku tofauti tofauti waliwakamata watu na mifugo ndani ya hifadhi hiyo.
Amesema kuwa watuhumiwa hao waliwaomba wamiliki wa mifugo na watu ambao walikutwa ndani ya hifadhi rushwa ili wasiwachukulie hatua za kisheria kama maadili ya kazi yanavyotaka, ambapo jumla waliomba na kupokea kiasi cha Sh. milioni 70,80,000.
Hata hivyo Kamanda huyo wa takukuru alieleza kuwa watuhumiwa wote wamekana makosa hayo, ambapo wote walirejeshwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana zao.