32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Askari wanaswa wakiiba mafuta ya ndege

MTZ Alhamisi new july.inddNa Veronica Romwald, Dar es Salaam

VITA ya kutumbua majipu kwa watumishi wa Serikali wasiokuwa waaminifu imeendelea kushika kasi, baada ya jana Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni kuagiza kusimamishwa kazi mara moja askari watatu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa tuhuma za wizi wa mafuta ya ndege na mizigo ya abiria.

Waziri Masauni alitoa agizo hilo jana wakati wa kikao chake na watendaji wa jeshi hilo, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Aliwataja askari hao kuwa ni Halfan Kisana, Mussa Mandauli na Abias Mwanza ambao walipangwa kwa ajili ya kazi maalumu uwanjani hapo.

“Mmenisomea ripoti yenu, nashangaa mmeshindwa kunifafanulia suala la wizi wa mafuta, mmekamata wezi wangapi na kiasi gani cha mafuta yaliyoibiwa. Ninazo taarifa kuwa baadhi ya askari wakiwamo hao niliowataja wanadaiwa kuhusika katika wizi huo.

“Nina taarifa kwamba Kisana na mwenzake Mandauli Oktoba 7, mwaka jana, saa mbili asubuhi wakitumia gari la Mkuu wa Kituo wa Jeshi la Zimamoto aina ya Landrover yenye namba za usajili ST 2948 walikamatwa lango la kuingia kikosi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), 603 KJ, wakiwa wamepakia madumu 10 yenye ujazo wa lita 20 yakiwa na mafuta ya ndege,” alisema.

Alisema tukio hilo liliripotiwa kituo cha polisi, lakini askari hao hawakuchukuliwa hatua zozote badala yake walipandishwa vyeo.

“Hii haiwezekani, nataka askari hawa wasimamishwe kazi na uchunguzi ufanyike haraka ndani ya siku 14. Maana rubani naye ni binadamu, anakwenda na kuweka mafuta kwenye ndege yake baadae anakuja kuiwasha na kuondoka akijua yapo mafuta ya kutosha, kumbe yameibwa bila yeye kujua, matokeo yake ndege inakwenda kuanguka, hatukubalini na suala hili, lazima hatua zichukuliwe dhidi yao ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema.

Katika hatua nyingine, ameliagiza jeshi hilo kuwatafuta wamiliki wa gari lenye namba za usajili T 225 AWM aina ya Saloon GX na gari lenye namba za usajili T 786 AWZ ambayo pia yanadaiwa kutumika kubeba mafuta ya wizi kwa nyakati tofauti.

Alisema gari lenye namba T 786 AWZ lilikutwa limebeba mafuta hayo Januari 8, mwaka huu, huku lenye namba  T 225 AWM lilibeba mafuta Januari 13, mwaka huu.

“Na hii yenye namba T 225 AWM nimeiona hapa uwanjani leo (jana), nataka wahusika wote watafutwe, wahojiwe na waeleze yale madumu yaliyokutwa kwenye magari yao walipeleka wapi mafuta, ikibainika wahusika ni askari wenyewe wachukuliwe hatua.

“Kwa sababu hatuwezi kufika mahala tukawa na watu wa usalama ambao nao ni wezi, nasikia kuna baadhi yenu hamtaki kukaguliwa, suala hilo nataka likome mara moja, vinginevyo hawa wanaokataa kukaguliwa wanaweza kutumiwa na watu kupitisha nyara za Serikali zilizoibwa.

“Awali nimewaeleza kwamba mnafanya kazi nzuri ya kulinda usalama, hawa wachache wenu watatuchafua, nimewataja hadharani ili wajue tunawajua na tutawashughulikia,” alisema.

Alisema askari mwingine, Abiasi Mwanza anadaiwa kushirikiana na mfanyakazi wa Kampuni ya Swisspot, Lucas Mwaganda kuiba mizigo ya abiria uwanjani hapo.

“Nina taarifa Agosti 26, 2014 saa 8 usiku, Mwanza na Mwaganda walinaswa na kamera za usalama (CCTV) wakiiba mizigo ya abiria iliyokuwa kule ‘Cargo’. Mwaganda aliingia na kuitoa mizigo hiyo kisha aliwasiliana na Mwanza ambaye alifika na pikipiki na kuichukua na kuondoka nayo,” alisema.

Alisema tukio hilo liliripotiwa polisi, hata hivyo Mwanza alihamishwa na kupelekwa makao makuu ya jeshi hilo ambako alipandishwa cheo na kuwa Inspekta.

“Pamoja na hayo, nataka muwasilishe ofisini kwangu ndani ya siku 14 mikakati yenu endelevu ya namna ya kuepukana na aibu hii kwa viwanja vyote vya ndege nchini.

“Upande wa Idara ya Uhamiaji, nimechukua ripoti yao nakwenda kuiangalia kuona kama mapato ya visa tunayopata yanaendana na idadi ya wateja wanaoingia nchini, maana tumepata taarifa kuna vijana wanataka kupata utajiri wa haraka haraka hapa, tutachunguza suala hili,” alisema.

Naye Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwenye uwanja wa JNIA, Martin Otieno, alisema wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali uwanjani hapo, ikiwamo upungufu wa askari.

“Tumefanikiwa kupunguza uhalifu, bado tunakabiliwa na changamoto ya wizi wa mafuta ya ndege, na tuna upungufu wa askari 99 kwa ajili ya kuimarisha ulinzi hapa uwanjani katika maeneo 31 tunayoyasimamia,” alisema.

Waziri huyo pia alikutana na maofisa wakuu wa jeshi hilo katika kikao cha ndani makao makuu ya jeshi hilo.

“Niliwaagiza kuwa wanatakiwa kuanzisha mara moja kitengo maalumu cha kupokea malalamiko ya wananchi,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles