Na MWANDISHI WETU
-CHUNYA
MKUU wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Maryprisca Mahundi, amesema vyombo vya dola vimeanza kufanya uchunguzi wa malalamiko dhidi ya askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilayani hapa anayedaiwa kuwatoza fedha wachimbaji wadogo wa madini kinyume cha sheria.
Aliyasema hayo baada ya kukamilika kwa kikao baina yake na wadau wa sekta ya madini wilayani hapa, ambacho malalamiko dhidi ya gharama zinazotozwa na askari huyo anayeliwakilisha jeshi hilo wilayani hapa lilichukua nafasi kubwa.
Mahundi alisema msingi wa kufuatiliwa kwa askari huyo kunatokana na agizo alilotoa Rais Dk. John Magufuli alipozungumza na wadau wa sekta ya madini Dar es Salaam hivi karibuni akitaka wachimbaji wadogo wanaozingatia sheria kutonyanyaswa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mahundi alisema kwa siku kadhaa sasa ofisi yake imekuwa inapokea malalamiko mengi kuhusu vitendo vya askari huyo na ndiyo maana iliamua kukiitisha ili kulitafutia ufumbuzi suala hilo na kuwawezesha wachimbaji wadogo kuendelea kufanya shughuli zao bila bugudha.
“Nimekuwa napokea malalamiko mengi sana kuhusiana na gharama hizi za huduma za Zimamoto. Wachimbaji wengine wanasema wanashinikizwa kutoa Sh milioni 12 kwa mwaka, wengine Sh milioni 6 kwa mwaka na wengine Sh milioni 3.
“Jambo la kusikitisha ni kwamba askari huyu anawatoza wachimbaji wadogo fedha ambazo hata hivyo hazitumiki kwa masilahi ya Serikali bali kwa masilahi yake binafsi, suala hili hatuwezi kukubali kuona likiendelea kutokea.
“Hivi karibuni tulimsikia Rais (Magufuli) akitoa agizo la kutonyanyaswa kwa wachimbaji wadogo wanaofanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria. Vitendo vya askari huyu vinakwamisha jitihada za Serikali za kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi wa ndani na nje,” alisema.