Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
UZAO wa pacha walioungana katika jamii ya Kimasai huchukuliwa kuwa ni laana kutoka kwa mababu. Familia iliyojaaliwa kupata pacha wa aina hiyo hutengwa.
Julai 12, mwaka huu Esther Simon, ambaye anatoka jamii ya Wamasai, alijaaliwa kujifungua pacha ambao aliwapa majina ya Precious na Gracious Mkono. Pacha hao alijifungua akiwa nyumbani, ambapo walikuwa wameungana sehemu ya tumboni.
“Nilipata hali ya uchungu nikiwa nyumbani, nilisaidiwa kujifungua na mama mkwe wangu, ni uzazi wangu wa pili, wa kwanza nilijifungua mtoto mmoja, uzazi wa pili ndiyo hawa pacha ambao bahati mbaya walikuja wakiwa wameungana,” anasema.
Anasema hakuamini alipojulishwa taarifa hiyo lakini aliamua kuwapokea kwa mikono miwili na kumshukuru Mungu akiamini amempatia pacha hao kwa ajili ya makusudi yake.
Anasema taarifa za uzazi wake huo zilipoenea kwenye jamii, wengi walishapatwa mshangao na kuwajadili wakidai ni laana.
“Sielewi kwanini jamii yangu inaamini kuzaa watoto wa aina hii ni laana, kila kona walikuwa wakizungumza na kujadili kwamba nimejifungua pacha walioungana, hii ni kwa sababu hawajawahi kuona watoto waliozaliwa wakiwa hivi, hata katika familia yetu hakuna historia ya aina hii.
“Baada ya kujifungua, tulichukuliwa pamoja na wanangu tukapelekwa zahanati kwa ajili ya kupata huduma zaidi, baadae tukahamishiwa Hospitali ya Kibaha kabla ya kuletwa huku Hospitali ya Taifa Muhimbili,” anasema.
Hali hiyo kitaalamu husababishwa na nini?.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Muhimbili, Petronila Ngiloi, anasema hadi sasa bado hakuna sababu za kitaalamu zinazoweza kutajwa kwamba ndio chanzo cha pacha kuungana.
“Hali hii hutokea wakati wa mgawanyiko wa seli ingawa si mara zote, kibaiolojia mbegu ya baba ikikutana na yai la mama ili kutengeneza mtoto huwa kunatokea mgawanyiko wa seli mara 18; sasa iwapo seli hizo hazikugawanyika na kuachana ikiwa mimba hiyo ni ya watoto pacha basi huzaliwa wakiwa wameungana baadhi ya viungo vyao,” anasema.
Anasema hali hiyo inapotokea wakati mwingine mtoto mmoja hukutwa akiwa amekamilika viungo vyote huku mwingine akiwa na kasoro kadhaa.
Historia
Hatua ya pacha hao kutenganishwa imeandika historia kwa Hospitali ya Muhimbili, Wilaya ya Kisarawe na jamii ya Kimasai kwa ujumla.
Dk. Ngiloi anasema hii ni awamu ya pili kwa hospitali hiyo kufanya upasuaji wa kuwatenganisha pacha walioungana.
“Imepita miaka 24, yaani kwa mara ya kwanza tulifanya upasuaji wa aina hii mwaka 1994 ambapo tulipokea pacha walioungana kutoka mkoani Shinyanga.
“Baada ya upasuaji pacha mmoja alifariki dunia baada ya siku 36, yule mwenzake tuliendelea kumfuatilia lakini baadae tulipoteana na hatujui hadi leo kama yupo hai au la,” anasema.
Anasema mwaka 1998 walipokea pacha wenye jinsi ya kike kutoka mkoani Lindi ambao walizaliwa wakiwa wameungana lakini hawakuweza kuwatenganisha na hivyo kuwapa rufaa kwenda nje ya nchi kwa matibabu.
Dk. Ngiloi anasema mwaka 2001 walipokea pacha wengine waliokuwa wamezaliwa wakiwa wameungana, wakitokea Rufiji mkoani Pwani. Pacha hao walipata rufaa kwenda nchini Afrika Kusini kwa matibabu ya kibingwa zaidi.
“Mtakumbuka pia Muhimbili tuliwapokea na kuwatibu pacha waliokuwa wameungana kutoka mkoani Iringa, Maria na Consolata ambao walifariki dunia wakiwa na umri wa miaka 29.
“Kuna pacha wengine wa jinsi ya kiume ambao tuliwapokea kutoka Mbeya, tuliwapa rufaa kwenda India kwa matibabu ambako walitenganishwa na hadi sasa wapo hai.
“Hivi sasa kuna pacha wengine ambao walifikishwa hapa hospitalini wakiwa wameungana hao tumewapa rufaa kwenda Saudi Arabia, madaktari wanaendelea kuwaandaa kwa upasuaji nadhani watatenganishwa wakati wowote kuanzia sasa.
“Baada ya hao, ndipo tukawapokea pacha hawa kutoka Kisarawe ambao walikuwa wameungana sehemu ya tumboni na tulipowafanyia uchunguzi kwa vipimo mbalimbali kikiwamo MRI na Ultra Sound tulibaini walikuwa wameungana sehemu kubwa ya ini,” anasema.
Upasuaji ulivyokuwa
Dk. Ngiloi anasema walitumia takriban saa sita kukamilisha upasuaji huo wa kihistoria wa kuwatenganisha pacha.
“Hapo tunahesabu muda wa upasuaji kuanzia pale tulipowapa dawa ya usingizi, muda wa upasuaji wenyewe na hadi walipoamka kutoka usingizi baada ya upasuaji, tunafurahi kuona kazi yetu imefanikiwa kwa kiwango kikubwa,” anasema na kuongeza:
“Lakini haikuwa rahisi, pacha hawa walizaliwa kijijini huko Kisarawe kwa njia ya kawaida, bahati nzuri wazazi walipoona wana hitilafu waliwapeleka hospitalini ndipo wakapewa rufaa kuja huku Muhimbili.
“Hadi kufika huku walikuwa wamechoka, walikuwa tayari wamepata infection (maambukizi) kwenye kitovu hivyo ilibidi tuanze kwanza kuwapa matibabu.
“Walipofika walikuwa na uzito wa kilo nne ilibidi pia tusubiri uzito wao uongezeke kidogo hadi walipofikisha kilo tisa kwa pamoja, yaani kila mmoja kilo 4.5 ndipo tukawatenganisha,” anasema.
Dk. Ngiloi anasema baada ya pacha hao kufikisha kilo hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alitoa ruhusa ya upasuaji kufanyika.
“Ilikuwa pia bahati nzuri kwani tulipokea ugeni wa mtaalamu wa upasuaji wa maini kutoka Ireland kipindi hicho, tukawafanyia upasuaji, wakatoka salama. Walikaa chumba cha uangalizi maalumu (ICU) kwa siku mbili na ya tatu hali zao zikaimarika.
“Tukaendelea kuwahudumia wodini na baada ya kuridhishwa na maendeleo yao ndipo tukamjulisha mkurugenzi kwamba tupo tayari kuwaruhusu kurejea nyumbani,” anasema.
Mapya yaibuka
Profesa Museru anasema taarifa hiyo ilikuwa njema lakini kabla ya kuwaruhusu kurejea nyumbani waliamua kujiridhisha kwa kutuma ofisa ustawi wa jamii wa hospitali hiyo kwenda kuangalia mazingira ya nyumbani kwao.
“Tulifanya hivyo ili kujiridhisha iwapo mazingira wanayokwenda kuishi pindi tutakapowapa ruhusa baada ya juhudi zote hizi kubwa tulizozifanya tangu walipokuja hapa hadi sasa walipofikia.
“Tuliona si vema kuwaruhusu bila kujiridhisha ili mafanikio haya makubwa tuliyoyapata yasipotee, walikwenda maofisa wetu lakini waliporudi wakuja kutueleza changamoto waliyobaini kule.
“Kwamba, mazingira ya makazi yao si rafiki kwa watoto waliofanyiwa upasuaji mkubwa kama huu, tukaona si vema kuwaruhusu waende kwani tusingekuwa tumewatendea haki pacha hawa.
“Kwenda kuishi kwenye mazingira ambayo si rafiki maana yake wangeweza kupata matatizo na juhudi zote tulizofanya ikawa hazijazaa matunda,” anasema.
Anasema tangu walipowapokea hadi sasa wamewahudumia bila gharama yoyote na kwamba hospitali imetumia takriban Sh milioni 34 kuwahudumia kwa mahitaji yao yote kama ambavyo sera inaeleza.
DC Jokate
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, hivi majuzi aliwatembelea wodini pacha hao kwa lengo la kuwasalimu.
“Ni wakazi wa wilaya yangu, nilikuja kuwaona na nikazungumza na uongozi wa Muhimbili, ni kweli katika jamii yao mtoto mlemavu au walioungana ni laana.
“Lakini tunafurahi kwamba kwa mafanikio ya upasuaji huu, inakuwa historia mpya kwamba watoto si laana bali ni baraka.
“Haijalishi wamezaliwa vipi, watoto hawa (Gracious na Precious) wamekuja na baraka kubwa mno kwa wazazi tunaamini hii itasaidia kubadilisha fikra ya jamii yao,” anasema.
UBA waguswa
Mkurugenzi Mkuu wa United Bank of Africa (UBA), Usman Isiaka, anasema mara ya kwanza waliposoma taarifa iliyoandikwa kuhusu pacha hao waliguswa kuwasaidia.
“Mama yao alieleza kwamba hawana bima ya afya hivyo hawezi kumudu gharama za matibabu, tukachukua hatua ya kuwasiliana na uongozi wa Muhimbili ukatujulisha kwamba hata makazi aliyonayo ni duni na si rafiki kwa ukuaji wa pacha hawa.
“Kwa kuwa ni wakazi wa Kisarawe, tulituma watu wetu kwenda kuonana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Jokate Mwegelo na tukakusudia kumjengea nyumba ya Sh milioni 16.08,” anasema na kuongeza:
“Pia tumewafungulia akaunti namba 560105600013396 kwa ajili ya kuwezesha makuzi yao ambayo tayari wafanyakazi wetu wamechangia kiasi cha Sh milioni mbili, tunawaalika na wananchi wengine wachangie kupitia akaunti hii,” anasema.