24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

ASILIMIA 70 WATUMIAJI DAWA ZA KULEVYA NI WANAWAKE’

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Siyanga, amesema zaidi ya asilimia 70 ya waathirika wa dawa za kulevya ni wanawake.

Amesema waathirika hao wanawake wamekuwa wakilazimika kuuza miili yao  waweze kupata fedha za kununulia dawa hizo.

Siyanga alitoa kauli hiyo  Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya ya mwaka 2016.

 “Zaidi ya asilimia 70 ya watumiaji wa dawa za kulevya ni wanawake… ndilo kundi lililoathirika zaidi, jambo hili ni kubwa si Tanzania tu, bali nchi mbalimbali duniani, tunahitaji ushirikiano  kuhakikisha tunalimaliza.

“Wengi wao ili wapate fedha za kununulia dawa hizo, wamekuwa wakilazimika kuuza miili yao jambo linalowafanya kupata magonjwa ya maambukizi ukiwamo Ukimwi,”alisema Siyanga.

Pamoja na mambo mengine, Siyanga alisema zipo njia tatu ambazo zinapaswa kufuatwa kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya inakomeshwa nchini.

Alizitaja mbinu hizo kuwa ni; kuzuia uingizaji, kutoa elimu na matibabu kwa waathirika huku akisisitiza kuwa  hawatachukulia hatua za sheria waathiriwa wa dawa za kulevya, badala yake watawasaidia kuwapatia tiba waweze kurejea katika hali yao ya kawaida huku wakiwahoji wanakopata dawa hizo.

 “Huwezi kupambana na waingizaji pekee ukafanikiwa, hapana, unaweza kuzuia baharini, lakini wakaingizia kupitia Msumbiji, ndiyo maana kote duniani wanatumia njia hizi hata zile nchi zenye adhabu kali bado wanatoa matibabu.

 “Elimu pia ni muhimu, kuielimisha jamii madhara ya matumizi ya dawa za kulevya nalo ni muhimu sana, ndiyo maana tumekuwa tukienda katika vyombo vya habari, tukifanikiwa haya mambo matatu kuyatimiza kwa pamoja, tutakuwa tumeiweza vita hii,”alisema.

Kuhusu vita hiyo ya dawa za kulevya ilipofikia, Siyanga alisema watawatumia waathirika kupata taarifa ya wapi wananunua dawa hizo, lakini hawatawachukulia hatua kali.

“Hivi unamkamata mtumiaji na kumpeleka gerezani, ndiyo utamaliza tatizo, hapana. Sisi tunawakamata hawa na kuwahoji watusaidie kupata taarifa ya wapi wanazinunua na tukimaliza kuwahoji, tunakwenda kuwapa matibabu na si kuwashikilia,” alisema Siyanga.

Mbinu hiyo ni tofauti na iliyotumiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipowataja wanaojihusisha na dawa za kulevya, ambako baadaye mahakama ilibaini ni watumiaji tu.

Kutokana na hilo, Kamishna wa Intelijensia wa Mamlaka hiyo, Fredrick Kibuta aliwakamata watu watano na wanaendelea na mahojiano zaidi.

“Hatuwezi kuwataja majina yao kwa sababu tunaendelea na uchunguzi, hawa watano ni wale wakubwa na kwa kuwa kabla ya kuwataja tunataka kujiridhisha.

“Ndiyo maana mnaweza kuona kama hatufanyi kazi lakini tuwahakikishie tunapambana vizuri,”alisema Kibuta.

Awali, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN), Alvaro Rodriguez, alisema suala la mapambano dhidi ya dawa za kulevya  linahitaji kuwa shirishi huku akiipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuanza mapambano ya vita hiyo.

“Katika mapambano haya  waathirika wakubwa wamekuwa wanawake hivyo tunaomba kutoa ushirikiano kwa kuwabaini wasafirishaji na wauzaji wa dawa hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles