Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Asasi za kiraia nchini zimetakiwa kushikamana kwa pamoja na kuhakikisha wanazisemea kazi wanazofanya katika taasisi zao ili kufahamika kwa wananchi na jamii kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango mkakati mpya wa Foundation For Civil Society (FCS) Rais wa Taasisi hiyo Dk. Stigmata Tenga amesema asasi za kiraia zinatakiwa kujengwa kwa kuwa ni mhimili wa maendeleo nchini na wananchi wanapaswa kuzifahamu.
“Tuisemee sekta hii na yale yote ambayo sekta hii inayafanya kwenye jamii, yasemeeni mnayoyafanya ili yajulikane msione aibu yeyote,”amesema Dk. Tenga.
Ameongeza kuwa asasi zinapaswa kutatua matatizo ya wananchi na kusaidia kuyaondoa,hilo ndio lengo kubwa la FCS katika dira yake.
“Tujenge uwajibikaji katika misingi ya ubinadamu na utu bila kujali kuna nini, bali kuwashirikisha wenzetu matatizo ambayo sekta ya asasi za kiraia nchini inapitia ambayo yanahitaji kutatuliwa kwani ni matatizo yanayojikita katika mifumo,” amesema.
Aidha amesema hawapaswi kutatua matatizo kwa mbinu za zamani ambazo si za kujenga mifumo bali ni mbinu za kutoa huduma.
“Tusipoangalia hivyo tutazidi kuona hizo mbinu zinaongezeka na kuwa kubwa sana na kuhakikisha wanaangalia mifumo ambayo ndio miundombiniu ya uwajibikaji ,” amesema
Kwa Upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga amesema kuwa wamezindua mpango mkakati mpya wa FCS ambao unalenga kushuka chini hususani vijijini katika kuwasaidia wananchi.
Amesema kupitia mpango huo taasisi yao itaendelea kufanya kazi na asasi mbalimbali za kiraia ambao ni wadau wao muhimu katika kuwafikia wananchi.
Amesema farsafa ya taasisi yao inaamini kuwa umasikini,hali ya kutokuwa na haki katika jamii,hali ya ukandamizaji watu wengine ni tatizo kubwa na ni adui wakubwa wa maendeleo.
Ameeleza katika rasilimali zao asilimia 90 inakwenda vijijini kuhudumia wananchi kila mwaka na waliopo Dar es Salaam ,taasisi nyingi zinaweza kufanya kazi na watu wengine kokote duniani,kuliko waliopo vijijini.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Asasi za Kiraia, Dk.Richard Samabiga ameipongeza FCS kwa hatua hiyo ya kuzindua mpango mkakati huo ambao unaonyesha dira ya kusaidia wananchi katika maeneo mbalimbali.
Amesema mpango huo unaleta matumaini makubwa kwa Asasi za kiraia katika kufanya kazi zao za kusaidia wananchi.
Mpango mkakati huo umejikita katika kutekeleza miradi ya utawala bora, usawa wa kijinsia na watu wenye ulemavu, kukuza uchumi na kujenga amani na utatuzi wa migogoro