Asha Bani, Dar es Salaam
Muungano wa Asasi za Kiraia zaidi ya 200 umekabidhi andiko lao kuhusu janga la virusi vya corona pamoja na mkakati wake wa utekelezaji.
Akikabidhi andiko hilo kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Faustine Ndugulile Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini (THRDC), Onesmo Olengurumwa amesema kwa kuzingatia majukumu ya msingi ya Azaki kuna maeneo mapana ambayo wamepanga kushirikiana na serikali ni pamoja na uhamasishaji wa umma kuzuia maambukizi, mabadiliko ya kimfumo na sera.
Mengine ni toaji wa huduma kama vile kuchangia vifaa tiba, elimu kwa umma vifaa vya usafi, utoaji wa misaada wa kisheria kwa waathirika, chakula, kisaikolojia, tafiti na tathmini za madhara.
“Ufuatiliaji na uangalizi wa utoaji wa huduma za afya, kushauri na kusaidia pale penye changamoto zinazojitokeza pamoja na mikakati mingine,” ameelekeza Olengurumwa.
Naye Naibu Waziri wa Afya, Dk. Ndugulile amesema changamoto za madaktari na wauguzi serikali inaendelea kutatua na kuhakikisha wanaagiza vifaa vya kutosha ili kujikinga na maradhi hayo.
“Tunafahamu kuna changamoto mbalimbali za kawaida lakini serikali imejipanga kuhakikisha tunapambana nazo ingawa uhitaji wa vifaa hivyo ni mkubwa.
“Changamoto ya vifaa kinga ni ya kidunia na si tu Tanzania na haikwepeki lakini sio sababu ya Watanzania kukosa huduma hospitalini kwa kuwa wahudumu hawana vifaa,” amesema.