30.4 C
Dar es Salaam
Friday, September 24, 2021

Kiza corona kuisha sasa

WAANDISHI WETU na MASHIRIKA YA HABARI YA KIMATAIFA

DUNIA ni kama imefunga milango, maeneo ambayo hapo zamani yalikuwa yakijaa misongamano ya watu wanaotafuta ridhiki za kila siku, yamebakia kuwa na sura kama maghofu.

Vizuizi vikuu vimewekwa kila mahali katika maisha ya wengi kuanzia kwenye kufunga shule, kuzuia kuzurura bila sababu na vile vya mikusanyiko ya watu.

Lakini je ugonjwa huu wa corona utaisha lini? na lini watu wataweza kuendelea na maisha yao kama ilivyo kuwa awali, ni swali ambalo wengi wanajiuliza.

Katikati ya wiki hii Shirika la Afya Duniani (WHO) lilionya kuwa watu wataendelea kuishi na virusi vya corona kwa muda mrefu.

Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom alikaririwa mapema wiki hii  akionya mapumziko ya kupambana na ugonjwa huo akisisitiza kuwa safari bado ni ndefu.

Mkuu huyo wa WHO  alisema kuna wasiwasi juu ya mwelekeo wa ugonjwa huo  hasa katika milipuko ya mapema katika sehemu za Afrika na kati na Amerika Kusini,  na kuonya kuwa “virusi vitakuwa na sisi kwa muda mrefu,”.

Kauli ya WHO kwamba virusi hivyo vinaweza kuchukua muda mrefu na pengine kuwa sehemu ya maisha ya watu  inaweza kupewa nguvu na Marekani ambapo Rais wake, Donald Trump alikaririwa kwamba nchi yake ingeweza kudhibiti ugonjwa huo hata kabla ya sikukuu ya Pasaka iliyoadhimishwa zaidi ya wiki mbili zilizopita na kwamba watu wangerejea katika shughuli zao kama kawaida lakini baadae alibadili kauli hio na kusema huenda watu wakarudi kwenye shughuli zao mwezi Mei.

Jana majimbo matatu ya Marekani yalianza kuruhusu baadhi ya maduka na saluni kufunguliwa.

Majimbo hayo ni Georgia na Oklahoma  wakati Alaska  ikiondoa vizuizi kwenye mighahawa  lakini ikiendelea na utaratibu wa kuzuia mikusanyiko.

Marekani imeanza kuchukua hatua hiyo si kwasababu ugonjwa huo umekwisha la hasha! bali baada ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, ingawa vifo katika taifa hilo sasa vimepita  51,000 na zaidi ikishika namba moja duniani.

Watalaamu wa afya nchini humo wanasema shughuli zinaweza kuanza kurejea taratibu na corona itakuwa sehemu ya maisha yao kama yalivyo magonjwa mengine hadi pale itakapopatikana kinga yake miezi 12 hadi 18 ijayo baada ya dawa nyingine kushindikana katika majaribio ya awali.

Hali ya Marekani ndiyo inayoakisi ile ya Uingereza sasa kwani Waziri Mkuu wake, Boris Johnson amesema anaamini Uingereza inaweza kugeuza wimbi la corona ndani ya wiki 12 zijazo lakini iwapo namba za kesi za virusi hivyo zinataanza kushuka.

Uingereza inabashiri kuwa maambukizi yanaweza kushuka  kwa miezi mitatu ijayo.

“ Basi kama ndivyo bado tutakuwa mbali na mwisho” anasema Boris na kuongeza;

“Inaweza kuchukua muda mrefu wimbi hili litoke, huenda ni miaka”.

Pengine kutokana na hali hiyo inaelezwa kuwa mkakati wa sasa wa kufunga shughuli za kijamii kwa sehemu kubwa utakuwa sio endelevu kwa muda mrefu kwa sababu mparanganyiko wa kiuchumi unaweza kuwa janga kubwa zaidi.

Hilo tayari limeshuhudiwa katika maeneo mbalimbali duniani, kwa mfano nchini Marekani tayari madai ya wasio na ajira yamefikia watu milioni 26au karibu asilimia 15 ya watu wake na tangu mwezi Machi, majimbo mengi ya Marekani yalikuwa kwenye presha kubwa ya kuanza kwa shughuli za biashara.

” Tunayo shida kubwa katika mkakati  gani wa kutoka na ni jinsi gani tunatoka katika hili,” anasmea Mark Woolhouse, ambaye ni profesa wa magonjwa ya kuambukiza kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh nchini humo.

“Si tu Uingereza, hakuna nchi yenye mkakati wa kutoka.” anasisitiza.

China ambako virusi hivyo vilianzia Disemba mwaka jana na kulazimika kufunga shughuli zake za uchumi mwezi Januari ili kujaribu kudhibiti hali ya maambukizi, shughuli zimerejea japo kwa kujikongoja lakini pia wamerejea huku tiba ya virusi hivyo ikiwa bado haijapatikana.

Watu walioko Shanghai wanasema, jiji hilo taratibu linarejea katika hali yake na sasa si lazima kwa watu wake kuvaa barakoa au kuzuiwa kwenda kufanya manunuzi au kutumia usafiri wa umma  na si lazima tena kwa maduka na migahawa kuwachukua watu kipimo cha joto kama ilivyokuwa ikifanyika awali.

Pamoja na hayo inaelezwa kuwa watu wamekuwa makini mno.

Mtu mmoja aliyezungumza na gazeti la The Guardian la Uingereza anasema wale tu unaowaona barabarani wasiovaa barakoa ni wanaume wazee, ambao hata hivyo hawakuwahi kutii sheria.

Zaidi ya watu milioni 2.5 duniani wameambukizwa virusi vya corona.

Karibu 178,000 wamepoteza maisha, huku robo ya vifo hivyo vikiwa ni kutoka Marekani, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.

Kutokana na janga la virusi hivyo, Umoja wa Mataifa umeonya kuwa njaa duniani inaweza kuongezeka mara mbili zaidi na kuwaweka watu milioni 265 katika hatari.

Australia inajaribu kujenga sapoti ya kimataifa kufanya mapitio mapya kufahamu virusi hivyo vilikotokea na vilivyosambaa.

Wakati Australia ikichukua hatua hiyo, Dawa ya kutibu corona iliyotengenezwa na kampuni ya Marekani imeshindwa kuonyesha mafanikio katika jaribio la kwanza.

Kumekuwa na matumaini makubwa kwamba dawa ya remdesivir ingeweza kutibu ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19.

Lakini jaribio la dawa hiyo nchini China limeonesha kuwa dawa hiyo haikufanikiwa, kwa mujibu wa waraka uliochapishwa kimakosa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Dawa hiyo haikuboresha hali za wagonjwa au kupunguza kiwango cha virusi katika damu, unasomeka waraka wa WHO.

Hata hivyo kampuni ya Marekani inayotengeneza dawa hiyo, Gilead Sciences, imesema kuwa waraka huo ulipotosha uchunguzi wake.

Aidha sambamba na hilo WHO imeonya kuhusu dawa iliyozinduliwa na Rais wa Madagascar, Andy Rajoelina kwamba inatibu virusi hivyo.

WHO imesema hakuna ushahidi wa dawa hiyo iliyotengenezwa kwa mmea wa ‘artemisia’ unaotumika kama chanzo cha kutibu malaria uliochanganywa na mimea mingine kama inatibu virusi vya corona.

Chuo cha Kitabibu cha nchini Madagascar Anamem nacho kimeonyesha shaka ya uwezo wa dawa hiyo kutibu virusi vya corona .

Dawa hiyo ya maji,Madagascar imesema itaanza kugawa bure kwa watu walio hatarini zaidi.

Hadi sasa watalaamu wanaamini iwapo watu zaidi watatengeneza kinga dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo au kubadili tabia katika jamii kutaweza kupunguza uwezo wa virusi hivyo kusambaa.

Wanasema ukiwafanya watu wako asilimia 60 wawe na kinga za kutosha, virusi hivyo haviwezi kusambaa.

Ingawa kuna taarifa kuwa dawa ya kutibu corona huenda ikawa imepatikana ndani ya miezi 12 hadi 18 ijayo iwapo kila kitu kitakwenda sawa kuanzia kwenye majaribio.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
157,854FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles