RAYMOND MINJA IRINGA
Kampuni ya Usindikaji maziwa ya Asas mkoani Iringa Asas imetoa msaada wa barakoa 500 kwa mama lishe wanaofanya biashara zao katika masoko matano yaliyoko manispaa ya Iringa kwa ajili ya kujinga na virusi vya corona.
Akikabidhi msaada huo Afisa Usalama, Afya Mazingira na Ubora wa Kampuni hiyo, Cosmas Charles kwa niaba ya mkurugenzi wa uzalishaji wa kampuni hiyo, Ahmed Salim Abri amesema huo ni mwendelezo wa kampuni hiyo katika kusaidia jamii ambayo inahusisha mikusanyiko ya watu wengi zaidi ndani na nje ya mkoa wa Iringa
Alisema kuwa msaada huo umewafikia mama lishe wanaofanya biashara katika masoko ya Mashine Tatu, Kihesa, Soko la kisasa la Mlandege, Soko Kuu la Iringa na soko la Ipogoro ambapo kuna mwingiliano wa watu wengi wanaopata mahitaji sokoni hapo.
Amesema kampuni ya Asas imekuwa na utaratibu wa kusaidia jamii bila kuchoka kutokana na hali za wananchi wengi sana kwa sasa kuhitaji msaada hivyo imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii hasa katika suala zima la kupambana kuenea kwa virusi vya corona mkoani humo na kuweza kutoa misaada mbalimbali kwa jamii yenye mikusanyiko ya watu.
Amesema kuwa msaada huo umewafikia mama lishe kutokana na kuwahudumia watu mbalimbali ambao wanatoka sehemu tofauti na kwa kuona changamoto yao baada ya kufanya utafiti na kubaini wengi wao wana uhitaji wa kupewa msaada wa barakoa bora.
Ameongeza kuwa kampuni hiyo imeshatoa msaada kwa umoja wa madereva daladala kwa kuwakabidhi vifaa kama ndoo maalumu za kunawia mikono, vitakasa mikono, barakoa zaidi ya 2000 kwa umoja wa madereva bajaji, na msaada wa mashine ya kujifukuzia kwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.