Raymond Minja, Iringa
Madereva wa bajaji katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wameweka vifaa vya kunawia mikono kwenye kila kituo ili kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona.
Utaratibu huo wa kunawa mikono unawalazimu abiria na madereva hao kuosha mikono kabla ya kupanda kwenye bajaji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Machi 19, wakati wa zoezi la kutoa msaada wa vifaa vya kusafisha mikono vipatavyo 300 kwa madereva bajaji, Ofisa wa Usalama Mahali pa Kazi kutoka kampuni ya ASAS, Cosmas Charles amesema kampuni hiyo imeamua kuunga mkono juhudi za serikali kupambana na virusi ugonjwa huo.
Vifaa vingine vilivyotolewa na kampuni hiyo ni ndoo za kunawia mikono zaidi ya 300, sabuni za kunawia mikono na tishu.
“Sisi Kampuni ya ASAS tumeona ni vema kujitolea vifaa hivi ili kuwasaidia watu wetu kuweza kujikinga kwa kusafisha mikono yao kwa maji na sabuni kwani kinga ni bora kuliko tiba,” amesema Cosmas.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa madereva Bajaji Iringa (UMBI), Norbert Sunka amesema msaada wa vifaa hivyo umekuja wakati mwafaka na kuahidi kuvitumia vema ili kujikinga na ugonjwa huo.