LONDON, ENGLAND
STAA wa muziki nchini Marekani, Ariana Grande, ameeleza kwamba yupo tayari kusaidia mazishi ya watu 22 waliopoteza maisha kutokana na mlipuko wa bomu, mara baada ya kumalizika kwa onyesho lake la muziki nchini Uingereza.
Watu 22 walipoteza maisha na wengine 119 walijeruhiwa kwa tukio la kigaidi la mlipuko wa bomu lililotokea kwenye Ukumbi wa Manchester Arena nchini Uingereza, ambapo msanii huyo alikuwa akifanya onyesho hilo ikiwa ni ziara yake ya muziki aliyoiita ‘The Dangerous Woman Tour’.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, msanii huyo amedai kuungana na familia za watu hao waliopoteza maisha ili atoe mchango wake wa kifedha katika mazishi yao.
“Nimefanya mazungumzo na familia za marehemu na nimewaomba nichangie katika shughuli za mazishi kwa kuwa marehemu wamepatwa na umauti baada ya kuhudhuria onyesho langu, nitaungana nao katika kipindi hiki kigumu kwao,” aliandika Ariana.