BERIN, UJERUMANI
KOCHA mpya wa klabu ya Bayern Munich, Carlo Ancelotti, ameweka wazi kuwa hana mpango wa kuja kuwa kocha wa klabu ya Barcelona au Atletico Madrid katika maisha yake ya soka.
Kocha huyo wa zamani wa klabu ya Real Madrid, aliwahi kuifundisha klabu hiyo kabla ya kujiunga na Bayern Munich, wakati yupo katika klabu hiyo alishinda katika mchezo wa fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid mwaka 2014.
Kocha huyo raia wa nchini Italia, amedai kuwa kama atakuwa na lengo la kufundisha soka nchini Hispania anaweza kurudi katika uwanja wa Santiago Bernabeu kwa ajili ya klabu yake ya zamani Real Madrid na si Barcelona wala Atletico Madrid.
“Nilikuwa katika klabu ya Real Madrid kwa miaka miwili na ninaamini nilifanya makubwa kwa kipindi hicho, lakini kwa sasa nipo nchini Ujerumani nikiwa na klabu ya Bayern Munich.
“Ninaamini nitafanya makubwa kama nilivyofanya Madrid kwa kuwa lengo langu ni kushinda mataji mbalimbali nikiwa na klabu hii.
“Kwa sasa sina mpango wa kutaka kujiunga na klabu nyingine hadi pale nitakapomalizana na klabu hii, najua zipo klabu nyingi ambazo zilionesha nia ya kutaka kufanya kazi na mimi kabla ya kujiunga na Bayern, lakini kwa sasa siwezi kuzizungumzia hizo.
“Katika mawazo yangu kwa sasa sidhani kama nitarudi tena nchini Hispania na kama nitapata nafasi ya kurudi huko basi labda katika klabu ya Real Madrid kwa mara ya pili lakini si klabu nyingine mbali na hapo.
“Najua kuna klabu kubwa kama Barcelona na Atletico Madrid ambazo zina wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa, lakini sina mpango wa kuzifundisha klabu hizo kwa sasa, lakini chochote kinaweza kutokea kwa baadaye,” alisema Ancelotti.
Kocha huyo tangu amejiunga na klabu ya Bayern Munich, anaonekana kufanya vizuri katika michezo yake ya mwanzo na amedai kuwa atahakikisha anachukua ubingwa wa ligi kuu pamoja na mataji mengine mbalimbali.
“Nashukuru kwa ushirikiano ambao ninaupata kwa sasa katika klabu hii, kutokana na hali hiyo, ninaamini nina nafasi kubwa ya kufanya vizuri kama vile kutwaa taji la ligi kuu na mengine, lakini kubwa ambalo ninaliangalia ni Ligi ya Mabingwa Ulaya.