NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM
UONGOZI wa timu ya Mansfield Town ya England, umemzuia mshambuliaji wake, Adi Yussuf, kujiunga na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa kile ilichodai ya kuwa nyota huyo ni majeruhi.
Yussuf ni miongoni mwa nyota 29 walioitwa kwenye kikosi cha Stars chini ya Kocha Charles Mkwasa, kitakachojiandaa na mchezo wa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2017 Gabon dhidi ya Nigeria ‘Super Eagles’ Septemba 5, mwaka huu.
Klabu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu nchini humo ilianza kupata hofu mapema juu ya straika huyo, 23, kuitwa kwenye kikosi cha Stars endapo angekubali uteuzi huo na kutimka.
Mtandao wa Chad.co.uk wa nchini humo, Alhamisi iliyopita uliripoti kuwa Mansfield imedai ina kikosi finyu na kumkosa Adi kungewapa pigo, huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Adam Murray, akidai bado nyota huyo anahitaji kufanya mazoezi ya kina na kikosi hicho kutokana na kukosa kipindi cha maandalizi ya msimu mpya ‘pre season’.
“Nataka aende huko kwa saa kadhaa na kurudi. Ni wazi haya mambo ni heshima nzuri kupata. Lakini tuna michezo ya kutakiwa kushinda na nitakuwa na mazungumzo na Adi…Tunamtaka kikosini kwetu. Ni mtu ambaye amekosa sehemu kubwa ya maandalizi ya msimu mpya, hivyo tunataka apate kasi yake,” ilisema taarifa ya kocha wake.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Celestine Mwesigwa, aliliambia MTANZANIA jana kuwa tayari wamepata barua rasmi kutoka Mansfield, wakidai hawataweza kumwachia mchezaji huyo baada ya kupata majeraha.
“Hakuweza kucheza mechi iliyopita. Klabu yake imetuambia katika kipindi atakachokuwa kwenye matibabu, hataweza kuuwahi mchezo huo, lakini wametuambia watakuwa tayari kumruhusu katika kipindi kingine atakachoitwa Stars,” alisema.
Hata hivyo, kwa mujibu wa upekuzi wa gazeti hili, Yussuf alikuwa ni miongoni mwa nyota 18 wa Mansfield waliotakiwa kucheza mechi iliyopita dhidi ya Notts County waliyoshinda mabao 2-0, aliwekwa benchi lakini hakuweza kutumika.
Mzanzibari huyo alikulia kwenye academy ya Leicester City, moja ya rekodi yake kubwa iliyompa heshima akiwa England ni kufunga mabao 27 katika mechi 39 wakati akiichezea Oxford City msimu uliopita.
Kikosi cha Stars kinachotarajia kuweka kambi ya siku 10 jijini Istanbul, Uturuki kinatarajia kujipima ubavu na Oman, Libya na Kuwait kabla ya kuivaa Nigeria jijini Dar es Salaam.