24.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

ANAYEDAIWA MWIZI WA BAJAJI AUAWA PWANI


NA GUSTAPHU HAULE, PWANI

WANANCHI wenye hasira katika Kata ya Pangani, Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani hapa, wamemshambulia na kusababisha kufariki dunia mtu mmoja anayedaiwa kuwa ni jambazi wa kupora pikipiki za miguu mitatu (Bajaji) katika maeneo yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Jonathan Shanna, aliwaambia waandishi wa habari wilayani Bagamoyo jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 2:30 usiku, likihusisha watu watatu ambao ni majambazi wa uporaji wa kutumia silaha mbalimbali.

Alisema kuwa majambazi hao watatu walifika katika eneo la stendi ya Mailimoja na walikodi Bajaji ili iwapeleke katika eneo la machinjio ya zamani yaliyoko Kata ya Pangani.

Kamanda Shanna alisema kuwa bajaji hiyo mpya yenye namba MC 415 BSH mali ya Zuhura Swed ilikuwa ikiendeshwa na dereva Alkumani Salehe (18) Mkazi wa Mwanalugali, Kata ya Tumbi.

Alisema kuwa walipofika eneo la machinjio, majambazi hao watatu walimkaba shingo dereva huyo na kisha kumjeruhi na kitu chenye ncha kali katika paja la mguu wa kushoto, kisha wakamfunga kamba na kumtupa porini na wao kutokomea na bajaji hiyo.

Baada ya majambazi hao kufanya unyama huo, walipita wasamaria wema katika eneo hilo la tukio na kumkuta kijana huyo akiwa amefungwa kamba, hivyo kumwokoa na kutoa taarifa polisi.

“Baada ya kupata taarifa hiyo, polisi walifanya doria kwa kufunga barabara zote na kuweka mitego sehemu mbalimbali na kuendesha msako kwa kuwashirikisha wananchi na hatimaye wezi hao waliingia katika mtego huo katika eneo la Kimele,” alisema Kamanda Shanna.

Hata hivyo, walimkamata mtu mmoja, huku wengine wakitokomea kusikojulikana. Lakini alifariki dunia wakati akikimbizwa hospitali kutokana na majeraha ya kushambuliwa na wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles