Timothy Itembe – Mara
JESHI la polisi mkoani lina msaka Mniko Chacha (20) mkazi wa Kijiji cha Kitagutiti Kata ya Mbogi Wilaya Tarime mkoani Mara kwa tuhuma za kumuua mdogo wake Hasaani Chacha (7), akidai anapendwa zaidi na baba yao.
Kamanda wa Polisi Tarime na Rorya, Henry Mwaibambe, akizungumza na waanishi wa habri jana, alisema tukio hilo lilitokea Juni, 26 saa saa 6 mchana wakati wakiwa machungani.
“Mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Kitagutiti, Hassani Chacha, alishambuliwa na kaka yake Mniko Chacha wakiwa wanachunga ng’ombe.
“Alimning’iniza juu mdogo wake na kumtupa chini mara mbili akihoji kwa nini anapendwa na baba yao kwa kuitwa mara kwa mara jikoni”alisema Mwaibambe.
Alisema marehemu alipoteza maisha akiwa katika Kituo cha Afya cha DK Steveni kilichopo Sirari ambapo alipelekwa ili kupatiwa matibabu.
Mtuhumiwa anadaiwa baada ya kutenda tukio hilo alitoroka na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Katika hatua nyingine, watu watatu raia wa China wamekamatwa wakiwa na madini ya aina mbalimbali ikiwamo dhahabu bila kibali.
Mwaibambe alisema askari wa usalama barabarani waliwakamata watu hao wakiwa na gari lenye namba KBW 5151 Toyota Cruiser na walipopekuliwa walikutwa na vifurushi vikiwa na madini.
“Juni 12 katika Barabara ya Sirari Musoma eneo la Nkende walikamatwa raia watatu wa China, walipopekuwa walikutwa vifurushi tisa vya salfeti na boksi moja vikiwa na mawe yanayodhaniwa ni madini.
“Walipohojiwa juu ya nyarakaza za hayo mawe na vibali hawakuwa navyo, taratibu zilifanyika sampuli zile zilichukuliwa na kupelekwa kwa maabara ya madini Dodoma ambapo majibu yalitoka na kubaini kuwa mawe hayo yana madini,”alisema Mwaibambe.