London, Uingereza
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitolea mwito kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, kuchunguza shambulizi la Israel dhidi ya jengo lililokuwa na ofisi za vyombo vya habari vya kimataifa na jingine ambapo watu 10 wakiwemo watoto wanane waliuawa.
Shirika la Amnesty limelitaja shambulizi hilo kuwa uhalifu wa kivita na kusema limesikitishwa zaidi kuhusu ongezeko la idadi ya vifo katika mji wa Gaza ambapo zaidi ya watu 180 wameuawa tangu mashambulizi kuanza.
Kupitia Ukurasa wa Mtandano wa kijamii “Twitter” shirika hilo limeandika kwamba mahakama hiyo ya kimataifa lazima ichunguze shambulizi la Israel dhidi ya kambi ya wakimbizi ya al-Shati iliyoko Gaza, ikiongeza kuwa mashambulizi dhidi ya raia ni uhalifu wa kivita.
Kulingana na Amnesty, mashambulizi ya Israel ni kama adhabu kwa raia wa Palestina.