24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Amina Salum Ali

Amina-Salum-AliNa Is-haka Omar, Zanzibar
BALOZI wa Umoja wa Afrika (AU) katika Umoja wa Mataifa (UN), Amina Salum Ali, amesema ana nia ya kuwania nafasi ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ingawa kwa sasa ni mapema kusema hivyo.
Balozi Amina ambaye amekuwa akitajwa kusaka kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu, aliweka msimamo huo wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano ulioitishwa na Jumuiya ya Kuhamasisha Maendeleo ya Wanawake Zanzibar (COWPZ) ambapo yeye ni mwenyekiti wake baada ya kurejea nchini kwa mapumziko ya muda mrefu.
“Ni mapema mno kuweza kusema kama nitagombea au la ingawa nina nia ya kufanya hivyo, ila naheshimu taratibu za chama changu,” alisema Balozi Amina ambaye pia aliwahi kushika wadhifa wa waziri wa fedha katika Serikali ya awamu ya tano iliyoongozwa na Dk. Salmini Amour Juma.
Alisema kwa sasa hawezi kuweka bayana msimamo wake kutokana na kuwa na mambo mengi ya kushughulikia na kwa kuwa ruhusa ya kufanya hivyo haijatolewa na chama chake ingawa anaamini kuwa ana sifa na uwezo wa kushika nafasi yeyote ya uongozi ndani ya Tanzania.
Amina ambaye aliwahi kuomba kuteuliwa kugombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho na kushindwa na Dk. Amani Abeid Karume (Rais wa Zanzibar wa awamu ya sita) mwaka 2000, alisema uzoefu alioupata ndani na nje ya chama hicho umemwongezea uwezo wa kushika nafasi ya uongozi wa dola kama inavyosisitizwa na mkakati wa maendeleo wa AU.

APONDA VIONGOZI SUK
Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, balozi huyo aliyeambatana na mwakilishi wa viti maalumu ambaye pia ni katibu wa COWPS, Mgeni Hassan Juma, alisema ni vyema ikaendelea ila kuna umuhimu kwa viongozi wa vyama vinavyoiunda wakaheshimiana na kutekeleza malengo ya kitaifa bila ya kuingiza hamasa na itikadi za vyama vyao.
“Ni nzuri na imekuwa ikitupatia sifa nje ya nchi, lakini inasikitisha kuona viongozi hawaonyeshi kama wao ni kitu kimoja badala yake hamasa za vyama vyao zinakuwa ndiyo mwongozo ambao hauleti tija na kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake,” alisema na kuwataka viongozi hao kujifunza kwa nchi nyingine katika kuuimarisha mfumo huo.

AZUNGUMZIA YA BURUNDI
Kuhusu hali tete inayojitokeza nchini Burundi, alisema jumuiya za kimataifa zinafuatilia kwa makini na hazitasita kuchukua hatua huku akiwataka viongozi wa bara la Afrika kuheshimu makubaliano kwa lengo la kuepusha machafuko ya kisiasa.
Alisema umoja huo tayari umechukua hatua za awali za kuzungumza na Rais Pierre Nkrunzinza kwa lengo la kumtahadharisha juu ya hatua anayotaka kuchukua baada ya umoja huo kupata taarifa za kiintelijensia kwamba kuna viashiria vya kutokea kwa vurugu katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo.
“Viongozi mbalimbali walikutana na Rais Nkurunzinza na kumtaka kuheshimu makubaliano ya Arusha ili kuepusha vurugu miongoni mwa wananchi wa nchi yake, lakini alipuuza bila ya kujali matokeo ya baadaye na ndiyo haya yanayoshuhudiwa sasa,” alisema Balozi Amina.
Aliongeza kuwa AU imeshindwa kuchukua hatua za ziada kutokana na kwamba Katiba yake haitoi nafasi kwa umoja huo kuingilia mambo ya ndani ya nchi husika iwapo haikiuki Katiba yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles