25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Amana yatoa huduma bure wakiadhimisha siku ya wanawake

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam na mikoa jirani wamenufaika kwa kupatiwa huduma za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali bure kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana katika kusherehekea siku ya wanawake duniani.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, Bryson Kiwelu, akipimwa presha na Muuguzi wa hospitali hiyo, Beatrice Ngenzi.

Huduma zilizotolewa ni pamoja na upimaji wa saratani ya matiti, saratani ya shingo ya kizazi, afya ya kinywa, macho, pua, koo na masikio, presha sukari, kutoa chanjo ya Uviko 19, kuchangia damu sambamba na uchunguzi maalumu kwa wajawazito.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Bryson Kiwelu, amesema wameamua kutoa huduma bure kurudisha fadhila kwa jamii wanayoihudumia.

Amesema kwa kiasi kikubwa huduma hizo zimetolewa na watumishi wanawake na kwamba wanajivunia kuwa nao wengi ambao ni zaidi ya asilimia 70 wakiwemo madaktari bingwa zaidi ya 10.

“Hapo awali ilikuwa ni nadra sana kuona kinamama kwenye fani ya udaktari na fani nyingine ngumu lakini sasa hivi mambo yamebadilika tuna wauguzi, madaktari, wataalam wa maabara, wataalam wa mionzi na huduma mbalimbali,” amesema Dk. Kiwelu.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Masikio, Pua na Koo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana, Fatma Kibao, akizungumza wakati wa utoaji huduma bure kusherehekea siku ya wanawake duniani.

Dk. Kiwelu amesema hospitali hiyo imefanya maboresho makubwa ya huduma mbalimbali ambapo wana madaktari bingwa zaidi ya 30 kwenye fani mbalimbali kama vile magonjwa ya ndani, uzazi, masikio, pua na koo, meno, upasuaji wa mifupa, figo, mfumo wa njia ya mkojo, ngozi na wengine.

Aidha amesema wanatarajia kuanzisha huduma za kipimo cha CT Scan na kusafisha damu na kwamba hivi sasa wanajenga jengo la kutolea huduma hiyo hatua itakayosaidia kupunguza adha ya watu kwenda Muhimbili au Mloganzila.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Masikio, Pua na Koo, Fatma Kibao, amesema utoaji huduma hizo umelenga kurudisha fadhila kwa jamii ili kuhakikisha inakuwa na afya salama.

“Tuliona tusherehekee kwa kurudisha fadhila katika jamii na jambo tulilolifanya haliangalii jinsia, tuliona sisi kinamama tujitoe tuweze kujua afya za Watanzania wenzetu, kinamama ndiyo watendaji wakuu, mama ndiyo injini ya kila mahali, mama asipokuwepo kila kitu kinatetereka,” amesema Dk. Fatma.

Mmoja wa wananchi waliojitokeza kupata huduma Mwanaidi Waziri, ameishukuru hospitali hiyo kwa kutoa huduma bure na kuzitaka hospitali zingine kuiga mfano huo kwani uhitaji wa huduma za afya ni mkubwa.

“Hatukutarajia kama kutatolewa huduma ya bure tumefurahi sana, kinamama tusikate tamaa tusonge mbele tusirudi nyuma,” amesema Mwanaidi.

Mwananchi mwingine Octaviana William ambaye alijitokeza kuchangia damu amesema ameguswa ili kuokoa maisha ya wajawazito na wagonjwa wengine wenye uhitaji wa damu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles