27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

Ally Saleh: Sitosahau mikasa niliyofanyiwa na SMZ

*Aapa kutoshirikiana na Mwakilishi wa  Malindi

*Aponda Bunge la Katiba limeacha historia mbaya

 

NA ELIZABETH  HOMBO, DODOMA

KATIKA tasnia ya  habari hapa Tanzania hususani kwenye utangazaji katika vyombo vya kimataifa ukilitaja jina la Ali Saleh ‘Ali Bato’ utakumbana na mwitikio mkubwa wa wananchi watakaotaka kufahamu yuko wapi mtangazaji huyu maarufu nchini.

Ali Sarehe akiwasilisha maoni ya upinzaniAli alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na umahiri wake katika utangazaji  akiwa mtangazaji katika Redio ya BBC Idhaa ya Kiswahili Swahili, akiwa mwakilishi wao upande wa Zanzibar.

Aliwavutia wengi kutokana na sauti na lugha yake adhimu ya Kiswahili lakini pia alivutia wengi kwani mtangazaji huyu anapotangaza humfanya msikilizaji wake anakuwa ni kama vile tukio analopewa taarifa analiona ‘live’

Ali amestaafu kazi ya utangazi mwaka 2013 na katika Uchaguzi Mkuu uliopita aliwania  Ubunge Jimbo la Malindi mjini Unguja kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) na kuchaguliwa kuwA mbunge wa Jimbo hilo.

Itakumbuka katika kazi yake ya utangazaji Ali ni miongoni mwa wanahabari waliopitia misukosuko mingi lakini hata hivyo ilimfanya kuwa ‘Strong’

Hivi karibuni MTANZANIA imefanya mahojiano na Mbunge huyo akiwa mjini Dodoma akihudhuria vikao vya Bunge na yafuatayo ni mahojiano hayo. Endelea…..

SWALI:  Tueleze historia yako ya uandishi wa habari

JIBU: Nilipenda uandishi tangu nikiwa mdogo. Nilikuwa napenda kusoma magazeti, kusikiliza radio. Nilianza kusikiliza BBC tangu nikiwa na miaka 12 na nilikuwa nikishiriki mashindano kadhaa yaliyokuwa yakifanywa na redio na nikawa nashinda baadhi ya mashindano.

Wakati nasoma sekondari nilikuwa nawahamasisha wenzangu kusikiliza redio. Nia yangu tangu mwanzo ilikuwa nifanye kazi mbili ya uandishi na sheria na vyote nikafanikiwa.
SWALI: Wewe ni miongoni mwa wanahabari wa kwanza Tanzania hasa Zanzibar, walioitangazia BBC  Idhaa ua Kiswahili ulipataje nafasi hiyo?
JIBU:Watangazaji wa mwanzo kutoka Zanzibar waliotangaza BBC walikuwa akina Nassor Malik na Zeyana Seif katika miaka ya 50 na 60 kisha wakaja kina Ahmed Rajab na wengine katika miaka ya 70 na kwa upande wa Tanzania Bara au Tanganyika walikuwa akina Jerome Kasembe na David Wakati, lakini wote hao walifanya kazi London.
Lakini kwa wale waliofanya kazi kutokea Zanzibar au Tanzania naamini ni akina Tido Muhando kwa upande wa Tanzania Bara na mimi kwa upande wa Zanzibar.
Kazi hiyo niliitafuta mimi mwenyewe maana ya kufanya kazi ya kuandika siasa na michezo katika magazeti ya Daily News na Uhuru. Nilikutana na Mwandishi mmoja wa BBC na kumueleza hamu yangu ya kufanya kazi nao na yeye akaniunganisha na kichekesho ni kuwa nilianza kwanza kuandika habari kwa Kiingereza katika kipindi cha Focus in Africa wakati huo ikiwa ni mwaka 1984 kisha ndio nikahamia Idhaa ya Kiswahili ya BBC.
SWALI: Wewe ni mwanahabari mtangazaji mwenye mvuto wa lugha adhimu ya kiswahili na ulipata mashabiki wengi wakikusikiliza kila ifikapo saa kumi na mbili jioni au asubuh nini siri yako?
JIBU: Mbali ya kulelewa katika mazingira mazuri ya kujua lugha ya Kiswahili na utamaduni wake lakini pia nimekuwa nikipenda Kiswahili sana. Na kwa sababu hiyo nimefanya juhudi kubwa kukielewa si tu kukizungumza bali pia kuandika. Matumizi yangu ya lugha katika uandishi wa habari ni kweli kama usemavyo imekuwa ndio silaha yangu kubwa ya kuvutia wasikilizaji na wasomaji wangu.
Nimekitumia kiswahili kujifundisha ushairi na nimetunga vitabu viwili vya mashairi vinavyoitwa ‘Changamka na Nemo’ Pia nimetunga kitabu cha hadithi fupi kinachoitwa JUMBA MARO na nimekamilisha kitabu changu kingine cha hadithi fupi kitachochapishwa karibuni kinachoitwa  ‘La kuvunda’  ambacho kitatoka karibuni. Pia nimefanikiwa kutunga kitabu cha mshairi na mtunzi maarufu aitwaye Haji Gora huko Zanzibar ambaye bila ya kwenda shule amefanikiwa kutunga vitabu 10. Kitabu chake pia kitatoka karibuni.
SWALI: Ulipata fursa ya kuongoza michezo kadhaa huko Zanzibar, unaweza kueleza kuhusu hili?
JIBU: Kwa sababu ya  kupata ulemavu sikuweza kuwa mchezaji wa mchezo wa mpira au soka ambao ninaupenda. Lakini kufidia hilo maisha yangu yote nimekuwa karibu na mchezo huo kwa njia ya uongozi na klabu ambayo nimeitumikia muda wote ni Shangani Sports Club ambayo nikiwa Katibu Mkuu tulipata ubingwa wa Zanzibar mwaka 1993/1994 na kushiriki michuano ya Kombe la Afrika Mashariki na Kati mwaka 1994 kule Sudan. Nimekuwa kiongozi katika Chama cha Mpira wa Kikapu Zanzibar, Chama cha Mpira wa Meza Zanzibar na pia Chama cha Chess Zanzibar na Tanzania. Nimetumikia vipindi viwili yaani miaka sita katika Baraza la Michezo Zanzibar (BMZ).
SWALI: Ulipata kukumbana na vitisho vingi wakati ule mara baada ya kumalizika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995 katika utawala wa Dk. Salmin Amour, hebu tueleze ilivyokuwa
JIBU: Ni kweli utawala wa Dk. Salmin ndipo mikasa mingi na uonevu yalinikuta kwa sababu ulikuwa ni utawala kandamizi sana. Nilizuliwa mashtaka kadhaa, nilipekuliwa mara kadhaa nyumbani kwangu na kwa ujumla nilikuwa nikifuatiliwa. Kazi ilikuwa ngumu na yenye vitisho. Kuna wakati nilikuwa naandika habari, ikitoka jioni asubuhi inayofuata nakimbia kwenda Dar es Salaam nakaa siku mbili tatu kusikiliza mshindo kisha ndio narudi Zanzibar.
Nimezuliwa mashtaka ya kushiriki katika hujuma za kulipua mtambo wa umeme pale Mtoni, nimezuliwa mashtaka ya kuwateka nyara wanawake wawili ambao walikuwa ni wapiga kura waliopenyezwa na CCM kutoka Matemwe kuja kupiga kura Kiembesamaki na nilikaa jela mwezi mzima nikishtakiwa kwa kushiriki maandamano ya kupinga Serikali.
Lakini pia nilifukuzwa kazi ya Serikali ambako nilikuwa nimeajiriwa kama Afisa Habari. Kwa ujumla sikuwa na amani kabisa katika kufanya kazi niliyoichagua na kuipenda ya kuandika habari.
SWALI: Ni kitu gani ambacho hutakisahau katika  maisha yako?
JIBU: Huwezi kuamini kwa sababu utaona kana kwamba nitasema kitu ambacho sikisahau ni moja ya mikasa ya dhuluma chungu nzima nilizofanyiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Mbali ya ile nilokwambia hapo mwanzo nimekumbuka na mwingine ambao nilikataliwa kuwa wakili huko Zanzibar kwa sababu za kisiasa hivyo elimu yangu ya sheria niliyoisoma UDSM sijaweza kuitumia.
Kwa kweli mkasa ambao sitousahau si wa kisiasa bali ni ule ambao ndio ulioniongoza kuweka nia ya kuwa Mwandishi na Mwanasheria. Ni tukio lililotokea nikiwa Pemba kwa Mzee na mlezi wangu Marehemu Sheikh Abdulrahman Ali Saleh huko Wete ambapo siku moja niliamua kuvuka bahari na kwenda sehemu inaitwa Mtambwe ambako ndiko anakotoka Maalim Seif Shariff Hamad na ukumbuke nilikuwa mtoto wa miaka 10.
Niliporudi mzee wangu alinitia adabu kwa kuondoka bila ya kuaga, si kwa kwenda Mtambwe. Nikapata funzo na yeye akaanza kujua kuwa mbegu ya mwanaye ni ipi na kusema kweli kuanzia hapo akiniongoza na nikajifunza mengi sana kwake.
SWALI: Unadhani ni kwanini viongozi wa Afrika hawapendi kuambiwa ukweli pale wanapoonekana wakikosea?
JIBU: Bado Afrika hakuna utamaduni wa utawala bora na demokrasia na tuko mbali kufikia azma hiyo, kama kweli imo ndani ya dhamira ya kisiasa. Maana yake ni kuwa viogozi wa Afrika hawafikiri kuwa utawala bora upo kwa faida ya amani na maendeleo. Bado viongozi wa Afrika wanaamini katika kutumia nguvu katika chaguzi, kutumia nguvu katika kuzuia maoni, kutumia nguvu hata katika kuleta maendeleo.
Afrika bado maana ya uongozi ni kutafuta maslahi binafsi na kujitajirisha wao na jamaa zao bila ya aibu yoyote.
Yote hayo na mengine yakifanywa bado viongozi hawa wa Kiafrika hawataki watajwe wala waguswe hata matendo yao yanapokwa dhahiri yanatishia maslahi hivyo kuanza figisu zao na waandishi wa habari.
SWALI: Ulikuwa mwanahabari aliyekuwa akikosoa Serikali ya SMZ pale inapokosea, unadhani umekuwa ukisikilizwa?
JIBU:Kwa kweli maoni yangu yamekuwa muhimu sana kwa Serikali ya Zanzibar na wakati mwingine hata Tanzania. Aina yangu ya uandishi muda mwingi ni ya utafiti na hivyo nikiandika habari huweka mwishoni maoni yanayoakisi fikra za umma juu ya jambo hilo lakini pia kuwa na usuli mzuri (background).

 

Taarifa zangu zimekuwa zikifuatiliwa mno na Serikali na naamini zimekuwa zikisaidia mara kadhaa kwa mfano kama siku moja nilipojua Mwalimu Nyerere alikuwa akisikiliza taarifa zangu pale nilipopata ki- note kutoka kwake mwaka 1985 kutaka nimueleze kwanini nilisema katika ripoti yangu kuwa Wazanzibari wengi wangependa Ali Hassan Mwinyi angeendelea kuwa Rais wa Zanzibar na si kuhamishwa au kupanda cheo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya miezi 18 ya mafanikio akifanya kazi pamoja na Maalim Seif Shariff Hamad.
Mwandishi akitaka ajue kuwa anasikilizwa na Serikali ni pale ambapo anapokuwa hakataliwi taarifa za wazi na za siri na wala hakataliwi mahojiano na afisa wa Serikali au mwanasiasa. Unapata heshima ya waziwazi na unavuka kile kiwango cha mwandishi wa kawaida. Ila katika kundi kubwa la waandishi wa habari ni wachache tu hufikia kiwango hicho na wao lazima walinde heshima hiyo.

SWALI: Ulistaafu lini kazi ya utangazaji?

 

JIBU: Nilistaafu mwaka 2013 baada ya kupata heshima ya uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete kuingia katika Tume ya Kukusanya Maoni Katiba ya Jaji Joseph Sinde Warioba. Kwa kuacha BBC niliacha moja kwa moja uandishi wa kila siku na badala yake kujikita kuandika makala katika magazeti mawili yaani Mtanzania na Sunday Citizen kama mchambuzi. Mbali ya BBC nimefanyia kazi pia Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW), Shirika la Kusambaza Habari la Reuters, gazeti la DIRA la Zanzibar ambalo lilipigwa marufuku na Serikali ya Zanzibar kwa kusimamia haki.
SWALI: Kitu gani unajivunia ambacho umekifanya ukiwa BBC ambacho kimeleta tija kwa taifa?
JIBU: Ni vitu vingi tu ikiwa ni pamoja na kufanya kazi katika chombo hicho maarufu na chenye nguvu duniani. BBC ni chombo ambacho maoni yake yanaheshimiwa na Serikali zote duniani na kuwa sehemu yake ni tija kwa taifa. Ile heshima ya kusikilizwa na maoni yangu kuheshimiwa ilitosha kuwa tija kwa taifa. Nimeandikia kuhusu mambo kadhaa na kuacha athari kubwa ikiwamo siasa na uchumi huko Zanzibar na hata Tanzania.
SWALI:Ulikuwa Kamishna wa Tume ya Warioba ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya Katiba mpya, unadhani ninyi kama tume mmetendewa haki kwani kazi mliyoifanya kuzunguka nchi nzima kukusanya maoni hayo inaonekana ni kama vile shilingi imetumbukia chooni?
JIBU:Kwa kweli ilivunja moyo sana kuona maoni mazuri ya Tume ya Warioba yalivyotupwa lakini baya zaidi ni pale maoni hayo yalipodharauliwa, kukebehiwa na kudharau heshima kubwa ya Jaji Warioba na kufanywa kana kwamba ni maoni yake binafsi na tena yaliyopotoka.
Vitendo vilivyopita katika Bunge la Katiba vitaacha historia mbaya sana nchini Tanzania na kwa fikra zangu tumetupa fursa nzuri ya kufikisha hatua nzuri suala la Muungano wa Tanzania ambapo mimi nadhani kwa sasa unapoteza haiba yake.
Lakini napata faraja kwamba pamoja na wenzangu tumeingia katika historia kufanya kazi ile muhimu kwa Taifa na kuwa historia itaweka nafasi nzuri kutumikia nchi yetu. Bado naamini kuna haja ya kurudi katika Mapendekezo ya Tume ya Warioba na si kupeleka Katiba Pendekezwa kupigiwa Kura ya Maoni na wananchi. Katiba Pendekezwa haitatufikisha mahali popote.
SWALI: Wewe ni mwanasiasa au mwanaharakati?
JIBU: Kwa sasa bado nipo katikati. Muda mwingi wa maisha yangu nimekuwa Mwandishi wa Habari ambaye ni mwanaharakati na hiyo ilitokana na jamii yetu kuwa na uonevu na dhulma nyingi. Hata sababu yangu ya kusomea sheria kuongeza na elimu yangu ya uandishi wa habari ilikuwa ni kujijenga kama mwanaharakati. Nimejifunza jinsi ya kutetea haki za wanawake kwa kuwa nilijiona nina uharakati ndani yangu.
Nimeandika makala kadhaa, nimewasilisha katika semina na makongamano kadhaa, nimezungumza katika midahalo chungu nzima nikiwa zaidi mwanaharakati kuliko mwandishi wa habari. Hivyo kwa kweli nipo katika kipindi cha mpito kutoka uanaharakati kwenda katika uanasiasa. Ila siamini kuwa ipo njia yoyote ya kumaliza uanaharakati wote ndani yangu maana upo ndani ya damu na hivyo nitalazimika kuweka mizania baina ya nguvu hizo mbili.
SWALI: Kwanini sasa uliamua kuingia kwenye siasa?
JIBU: Maisha yangu yote nimekuwa mwanasiasa nje ya ulingo wa siasa. Nimekuwa na siasa ndani ya muda wangu ambayo ilikuwa ikingojea muda tu halisi wa kujitokeza. Sijui kama nimechelewa au ndio kudra ya Mungu aliyenituma nijidhihirishe wakati huu.Kwa wengi walionielewa hawakuweza kabisa kunitenga na siasa kama ambavyo wengi hawakuweza kuamini kuwa mimi sikuwa mwanachama wa CUF.
Kabla ya kuingia kwenye siasa mwenyewe nimesaidia sana wanasiasa katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na ushauri. Wengi walijisikia wepesi kunifuata na kutaka ushauri wangu katika mambo kadhaa na ndio maana hata hapa bungeni wengi hawaamini kuwa mimi ni mbunge mgeni.
Baada ya kufanya siasa nje ya siasa, ijapokuwa tangu mfumo wa vyama vingi, nimekuwa nikiombwa niingie katika siasa kugombea Jimbo la Mji Mkongwe, lakini nilipenda zaidi kazi yangu ya uandishi wa habari. Baada ya kuacha BBC ndipo nilipoanza kufikiria kuingia siasa moja kwa moja na bahati nzuri chama change cha CUF kikanikubali na kunipa baraka zake na wananchi wa Jimbo la Malindi wakaniamini na kunipa kura nyingi.
SWALI: Jimbo Malindi  lina historia nyingi ikiwamo majengo ya kihistoria Kanisa la Mkunazini, lililokuwa soko la watumwa, Jumba la Ajabu maarufu Beit el Jaib, Je vivutio hivi vinaleta tija kwa Wazanzibari?
JIBU: Ni kweli Jimbo la Malindi ni jimbo muhimu kwa Zanzibar na ndio jimbo tajiri kuliko zote Zanzibar kwa vyanzo vya mapato na fursa nyingi za ajira na nyinginezo. Mawazo yangu kuwa tunaweza kutumia fursa hizo kwa faida ya jimbo.
Tutakachofanya ni kuwaelewesha wale wote waliowekeza katika jimbo letu kwamba wana wajibu wa kurudisha sehemu ya faida yao kwa jamii inayowazunguka na fedha kama hizo tutazitumia kwa miradi ya maendeleo na kujenga ustawi wa wana Malindi.
SWALI: Unadhani utawezaje kufanya kazi na Mwakilishi wa CCM?
JIBU: Bila ya shaka sitafanya kazi kabisa na huyo anayeitwa Mwakilishi wa Jimbo la Malindi. Mwakilishi wetu wa jimbo mwenye ridhaa ya umma ni Ismail Jussa aliyeshinda kwa kura nyingi hapo Oktoba 25, 2015.
Mtu aliyepora kura na kushiriki katika Uchaguzi wa Marudio uliokosa uhalali wa kisheria na kikatiba, siwezi kabisa kumpa ushirikiano wangu na naamini pia atakataliwa na wananchi wa Jimbo la Malindi.
SWALI: Nini vipaumbele vyako katika  kipindi cha miaka mitano ijayo?
JIBU:Jimbo la Malindi ni jimbo la mjini lakini bado lina matatizo kama majimbo ambayo hayako mjini, ila kuna mengine ni mahsusi kwa majimbo yaliyo mjini kama vile ukosefu wa ajira na tatizo la matumizi ya dawa za kulevya. Maeneo haya ni ya kipaumbele kwangu.
Pia kuna tatizo la ukosefu wa maji ambalo pamoja na Serikali kujisifu kuwa maji yapo kwa asilimia 80 kwa maeneo ya mjini, bado tatizo ni kubwa na ni jambo ambalo linafaa kukabiliwa kwa nguvu ingawa sidhani kuwa bila ya kuingiliwa na Serikali tatizo hilo linaweza kumalizwa kabisa.  Hili pia ni kipaumbele kwangu.
Kuna eneo la kuwapa nguvu za kiuchumi kinamama na kusaidia pia eneo la elimu kwa vijana wanaomaliza masomo na kuwapo haja ya kuwapa ujuzi ili waweze kujitegemea na katika muda wangu nitalipa kipaumbele.
SWALI: Unadhani serikali ya Dk. Shein itaweza kumaliza kero za wananchi ikiwamo kuwaondolea umaskini ilhali pato la Zanzibar  liko chini lakini pia baadhi ya nchi wahisani kutangaza kusitisha misaada baada ya kutokubaliana na matokeo ya uchaguzi wa marudio?
JIBU: Sidhani kuwa Serikali ya Dk Shein inaweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi huko Zanzibar na kama angekuwa na uwezo huo tungeona mabadiliko hayo katika kipindi chake cha uongozi halali cha 2010/2015 ambapo hatukuona uchumi kupanda kiasi hicho wala ajira kutengenezwa kupunguza tatizo na wala uwekezaji kustawi kwa faida ya Zanzibar.
Ni wazi CCM ilikosa sera imara zenye maslahi kwa Zanzibar na ndio maana CUF tuliungwa mkono na wananchi pale tulipokuja na sera mbadala wakati wa Kampeni za Uchaguzi 2015. Kuipeleka Zanzibar sawa na anga za nchi yenye mafanikio makubwa kama Singapore ndicho tulichokiuza kwa wananchi ambao walimpa Maalim Seif ridhaa ya kuiongoza Zanzibar lakini akafanyiwa hiyana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar, Jecha Salim Jecha.

 

CCM Zanzibar na Dk Shein hawana ubunifu wa kuleta mabadiliiko Zanzibar na sitarajii kuwa uongozi wake utaleta mabadiliiko yoyote ya maana kwa Zanzibar ambayo inapaswa kusimama kwa miguu yake wenyewe ili angalau kufanana na nchi ndogo kama sisi kama vile Seychelles, Mauritius, Qatar au Singapore au kufikia katika kiwango angalau cha robo ya mafanikio yao.
Tuliposema tunataka kuipeleka Zanzibar kufanana na Singapore ni Dk. Shein mwenyewe aliyesema kuwa haiwezekani lakini mwisho yeye mwenyewe akaja na maneno kuwa ataigeuza Zanzibar kuwa Dubai ya Afrika. Sasa mtu mwenye aina hii ya fikra sidhani kama anaweza kuiletea jamii mabadiliko ya kweli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles