24.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

ALIYEUA FAMILIA KWA JEMBE AKAMATWA ADAI MKEWE ALIZAA NJE YA NDOA

Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imemkamata Ammy Lukule, anayetuhumiwa kumuua mkewe, Upendo Lukule, shemeji yake Magreth Samuel na mtoto wa chini ya mwaka mmoja kwa kutumia jembe.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, amesema mtuhumiwa amekamatwa mkoani Iringa alikokuwa amejificha.

Alidai kuwa baada ya mahojiano, mtuhumiwa huyo alikiri kufanya mauaji hayo baada ya kubaini kwamba mkewe amezaa mtoto mmoja nje ya ndoa.

Mtuhumiwa huyo ambaye ni Mhasibu wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, anadaiwa kufanya mauaji hayo usiku wa Januari 4 katika eneo la Kimara, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mambosasa alisema: “Tumefanikiwa kumnasa mtuhumiwa Lukule mkoani Iringa na taratibu zinaendelea kumrejesha Dar es Salaam.

“Katika utetezi wake wa awali amedai mke wake amezaa mtoto mmoja wa nje ya ndoa.”

Siku moja baada ya kutokea kwa tukio hilo, Benedict Kitalika, aliyekuwa akikaimu nafasi ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema muuaji alifanya tukio hilo usiku wa Januari 4 na kisha kutokomea kusikojulikana.

Kamanda Kitalika, alisema kuwa mwanaume mmoja ambaye anafanya kazi ya uhasibu katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, aliyejulikana kwa jina la Ammy Lucas Lukule, anadaiwa kumuua mke wake, mtoto na shemeji yake.

Inasemekana kulikuwa na ugomvi kwamba mwanamume alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa mtoto mdogo si wake na anajihusisha na mapenzi na wanaume wengine, hivyo aliamua kuwaua kwa jembe na kukimbia.

Alisema baada ya kufanya tukio hilo, anadaiwa kuwa aliacha ujumbe kuwa polisi wasihangaike kwani yeye ndiye kafanya mauaji.

Polisi walisema taarifa za tukio hilo walizipata kutoka kwa majirani baada ya kugundua hakuna dalili ya kuwapo watu kwenye nyumba hiyo na kuanza kuchunguza, ndipo walipogundua hayo na kuita polisi kuvuja mlango.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles