NA FRANCIS GODWIN
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, aliyefukuzwa uanachama kwa usaliti wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015, Dk. Jesca Msambatavangu, amekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumvamia mwanamke mmoja na kumfanyia vitendo vya kinyama.
Moja ya kitendo kinachodaiwa kufanywa na Jesca, ni kumchoma mwanamke huyo sindano inayodhaniwa kuwa ya sumu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi, alisema Jesca alikamatwa jana mchana, baada ya jeshi hilo kupokea taarifa ya tukio.
“Tunamshikilia Jesca Msambatavangu kwa tuhuma za kumvamia na kumpiga mwanamke mmoja wa kibwabwa katika Manispaa ya Iringa.
“Inaonekana mwanamke huyu ameumizwa sehemu mbalimbali za mwili wake na inadaiwa walimchoma sindano inayodhaniwa kuwa ya sumu,”alisema Kamanda Mjengi.
Alisema mwanamke huyo, jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiusalama, alivamiwa na watu wanne akiwemo Jesca.
Alisema mpaka sasa wanaendelea na msako mkali wa kuwasaka watuhumiwa wengine watatu ambao (majina yao yamehifadhiwa), kwa sababu wanadaiwa kuhusika katika tukio hilo.
“Tunawaomba wananchi wa mkoa huu, watoe ushirikiano wa kuwafichua watu hawa haraka ili wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria, hatuwezi kukubali matukio ya aina hii yaendelee katika jamii yetu,”alisema.
Itakumbukwa kuwa baada ya kufukuzwa uongozi na vikao vya juu vya CCM, Jesca alitangaza kutojihusisha tena shughuli zozote za siasa kwa kuwa yote yaliyotendeka ndani ya chama chake, amemwachia Mungu.