31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Alie juu mfuate huko huko

Pg 32*Simba yaitandika Ndanda na kuishusha Yanga kileleni

NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

TIMU ya soka ya Simba jana ilirejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kishindo baada ya kuinyuka Ndanda FC mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo ya ushindi wa jana yameiwezesha Simba kufikisha pointi 51 na kuwashusha mahasimu wao wa jadi Yanga hadi nafasi ya pili, wakiwa wamejikusanyia pointi 50 huku Azam FC wakibaki nafasi tatu na pointi 47.

Simba wamerejea kileleni kwa kuwazidi mahasimu wao Yanga kwa pointi moja, lakini Wanajangwani hao wapo nyuma kwa mchezo mmoja kutokana na kushuka dimbani mara 21 huku wapinzani wao wakicheza mara 22.

Mabao ya Wekundu hao wa Masimbazi ambao walitawala mchezo kwa vipindi vyote, yalipachikwa wavuni na kiungo Mwinyi Kazimoto dakika ya 36 huku mshambuliaji Hamis Kiiza akifunga dakika ya 57 na 72.

Mchezo huo ulianza kwa timu ya Ndanda ikionekana kukaba vizuri, ili kutoruhusu bao la mapema lakini dakika ya 27 Said Ndemla na Justice Majabvi walikosa bao la wazi baada ya kushindwa kuunganisha vyema mpira wa krosi uliopigwa na mlinzi Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Simba ilibadilika na kuanza kasi yao kwa kulisakana lango la Ndanda bila mafanikio dakika za mwanzo, lakini walifanikiwa kutikisa nyavu za wapinzani wao dakika ya 36 kupitia kwa Kazimoto aliyepiga shuti kali akiunganisha vyema krosi iliyochongwa na Ibrahim Ajib.

Bao hilo lilidumu hadi kipindi cha mapumziko ambapo Simba walitoka uwanjani wakiwa mbele kwa bao moja.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa  Ndanda kufanya mabadiliko kwa kumtoa Omega Seme na kumwingiza Bryson Raphael, ambapo dakika ya 57 Kiiza aliandika  bao la pili kwa Simba kwa kichwa akiunganisha mpira wa kona safi iliyochongwa na Ajib.

Baada ya kufungwa mabao hayo, Ndanda walicharuka na kutengeneza nafasi za kufunga, lakini walishindwa kupachika mabao kutokana na ubutu wa safu ya ushambuliaji.

Dakika ya 53 Simba walifanya mabadiliko ya kumtoa Ndemla na nafasi yake kuchukuliwa na Awadhi Juma, huku Ndanda wakimtoa Omari Mponda na kumwingiza Salum Mineli.

Mabadiliko hayo yalizaa matunda kwa upande wa Simba, ambapo dakika ya 72 Kiiza alifunga bao la tatu akiunganisha kiulaini pasi ya Daniel Lyanga aliyeunasa mpira uliotemwa na kipa Jeremia Kisubi.

Mshambuliaji huyo raia wa Uganda amefikisha jumla ya mabao18 katika Ligi Kuu na kumwacha Amissi Tambwe wa Yanga aliyefunga 17.

Dakika ya 74 Simba walifanya tena mabadiliko ya kumtoa Kazimoto na kumwingiza Mussa Hassan ‘Mgosi’, huku Ndanda wakimtoa Kigi Makasi na nafasi yake kuchukuliwa na Ahmad Msumi.

Simba: Vincent Agban, Hassan Ramadhan ‘Kessy’, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Jjuuko Murshid, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto/Mussa Hassan ‘Mgosi’, Jonas Mkude, Hamis Kiiza, Ibrahim Ajib na Said Ndemla/Awadhi Juma.

Ndanda: Jeremia Kisubi, Azizi Sibo, Paul Ngalema, Kassian Ponera, Salvatory Ntebe, Hemed Khoja, William Elias, Omega Seme/Braison Raphael, Omari Mponda/Salum Mineli, Atupele Green, Kigi Makasi/Ahmad Msumi.

Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliochezwa katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya wenyeji Mbeya City waliichapa Stand United ya Shinyanga mabao 2-0.

Mabao ya Mbeya City yaliwekwa wavuni na Raphael Alfa dakika ya 13 kipindi cha kwanza na Haruna Shamte dakika ya 48 kipindi cha pili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles