Na SHARIFA MMASI-DAR ES SALAAM
HIVI karibuni, nyota wa kikapu Tanzania, Hasheem Thabeet alizua gumzo kwa wadau mbalimbali wa mchezo huo, baada ya kuanika hadharani usajili wake na moja ya timu zinazoshiriki Ligi ya Kuu ya Kikapu nchini Japan, Yokohama B-Corsairs.
Nyota huyo aliyezaliwa Februari 16 mwaka 1987, amewahi kuzichezea timu kadhaa zinazoshiriki Ligi Kuu ya NBA nchini Marekani kama vile, Houston Rockets, Oklahoma City Thunder, Memphis Grizzlies na zingine kabla ya kushuka kiwango na kushiriki Ligi ndogo (Development League) ya nchini humo.
Alfred Ngalaliji ni mkufunzi wa mpira wa kikapu ngazi ya Taifa hapa nchini, anazungumza na  SPOTIKIKI, juu usajili wa mchezaji huyo na mambo mbalimbali yanayohusu muelekeo wake nchini Japan.
Spotikiki: Una tetesi zozote juu ya nyota wa Tanzania Hasheem Thabeet kumwaga wino kwenye moja ya klabu inayoshiriki Ligi Kuu ya Kikapu nchini Japan?
Ngalaliji: Sinaushahidi wa kutosha, ingawa  nimeona picha zake zikiashiria kitu kama hicho.
Spotikiki: Vipi kama ukijihakikishia amemwaga wino kwa ajili ya kuitumikia Yokohama B-Corsairs inayoshiriki ligi hiyo?
Ngalaliji: Kwake yeye litakuwa jambo jema ila kwa sisi tunayemtazama na kumfuatilia, sidhani kama atakuwa amefanya maamuzi sahihi katika kukuza na kuendeleza kikapu chake.
Spotikiki: Unakitu chochote cha kuzungumzia maisha ya nyota huyo kipindi yupo NBA na kuondoka kwake?
Ngalaliji: Unajua wakati  akiwa NBA alicheza msimu mmoja tu na ule uliofuata hakuwa na mafanikio yoyote ndani ya klabu, hivyo watawala wa timu ikabidi wamrudishe kwenye ligi ndogo (D-League) ili acheze kwa kiwango, ndipo wampandiishe daraja sambamba na kuingia naye mkataba.
Spotikiki: Kutokana na uzoefu pamoja na ukongwe ulionao kwenye mpira wa kikapu, unadhani kwanini hakufanya vema ligi ndogo ili apande NBA?
Ngalaliji: Asikuambie mtu, ligi ndogo siku zote inakuwa ngumu kwasababu kila mchezaji anahitaji kuonyesha kiwango chake ili apande daraja, pamoja na Thabeet kuwahi kukodisha wakufunzi wamsimamie mazoezi, lakini bado kiwango chake hakikuonekana.
Spotikiki: Wakati Thabeet anaichezea timu ya Grand Rapids inayoshiriki ligi ndogo, kupitia mashindano maalumu ya kusaka vipaji ‘Summer League’ aliripotiwa kufanya tukio la kuvunja viti ndani ya chumba cha kubadilishia nguo, unafikiri hiyo ni miongoni mwa sababu zilizomnyima ulaji timu za NBA?
Ngalaliji: Unajua unapokuwa mchezaji mkubwa mwenye jina kama yeye, lazima jopo la watu likufuatilie, sitaki kuhukumu kwa kile kilichomtokea Grand Rapids, isipokuwa inawezekana hiyo nayo ikawa sababu kwa wenye timu zao.
Spotikiki: Yanasemwa mengi kutoka midomoni mwa wadau wa kikapu nchini juu ya mchezo huo kupotea kabisa, kwenye ulimwengu wa kikapu, baada ya kujichimbia Japan, kwako wewe unalitizama hilo kwa jicho gani?
Ngalaliji: Waswahili wanamsemo wao usemao kuwa ‘Lisemwalo lipo kama halipo basi laja’, mimi naona tumpe muda kila mmoja wetu atajionea.
Spotikiki: Upi wito wako kwa nyota huyo?
Ngalaliji: Aendelee kujituma, hata uko aliko sasa kuna wachezaji wengi wenye viwango na kila mmoja atahitaji kuonyesha uwezo wake ili afike mbali.
Spotikiki: Ushauri wako kwa wachezaji wa mchezo huo hapa nyumbani ni nini?
Ngalaliji: Vijana watulize akili kwa kucheza mpira wa kikapu kwa kuzingatia sheria na kanuni ili wafikie malengo, mbali na hilo niwatake wale ambao wamefanikiwa kusajiliwa na timu mbalimbali barani Afrika kuzitumia vema nafasi hizo ili waitangaze Tanzania.