25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Al Bashir kufikishwa mahakamani wiki hii

KHARTOUM, SUDAN

MWENDESHA Mashtaka mkuu nchini Sudan, Al Waleed Sayyed Ahmed amesema kiongozi aliyeondolewa madarakani, Omar al-Bashir atafikishwa mahakamani wiki ijayo.

Ahmed aliwaambia waandishi wa habari kwamba al-Bashir anakabiliwa na mashtaka ya rushwa na kumiliki fedha za kigeni kinyume cha sheria.

Hayo yanatokea baada ya zaidi ya miezi miwili tangu jeshi lilipomwondoa Bashir madarakani kufuatia maandamano makubwa ya kitaifa yaliyopinga utawala wake. 

Siku ya Alhamisi wiki iliyopita, ofisa mmoja alinukuliwa na shirika la habari la Sudan (SUNA), akisema al-Bashir anakabiliwa pia na mashtaka ya kuamuru hali ya dharura nchini Sudan.

Mnamo Aprili mwaka huu, mkuu wa jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alisema fedha zaidi ya Dola milioni 113 za kimarekani zilikamatwa kutoka kwenye makazi ya al-Bashir. 

Jenerali Burhan alisema polisi, wanajeshi na mawakala wa usalama walipata kiasi cha Euro milioni saba , Dola za Kimarekani 350,000 na Pauni za Sudan milioni moja na tano.

Fedha hizo zilikamatwa kwenye kasri la al-Bashir ambaye alitangaza hali ya dharura Februari 22 katika jitihada za kuyazima maandamano yaliyoanza tangu mwezi Desemba mwaka jana.

Wakati w atangazo hilo, al-Bashir alitoa alipitisha amri kwamba ni kinyume cha sheria kwa mtu kuwa na fedha za kigeni zaidi ya Dola 5,000.

Mwezi uliopita, mwendesha mashtaka mkuu Ahmed aliamuru al-Bashir ahojiwe kuhusu tuhuma za utakatishaji fedha na kufadhili ugaidi. 

Mnamo mwezi Mei, mwendesha mashtaka huyo  alisema Bashir atashtakiwa kwa mauaji ya waandamanaji waliokuwa wanaipinga serikali yake jambo lililosabisha kuondolewa kwake madarakani.

Ahmed alisema watuhumiwa wengine waliotumikia chini ya utawala wa Bashir bado wanachunguzwa.  

Ingawa hakuwataja majina lakini alisema tuhuma dhidi yao ni kuhusu umiliki wa ardhi.

Maandamano dhidi ya utawala wa al-Bashir yalianza Desemba 19 mwaka jana baada ya serikali yake kupandisha bei ya mkate. 

Al-Bashir aliondolewa madarakani na jeshi Aprili 11 mwaka huu baada ya maelfu ya waandamanaji wakiongozwa na muungano wa vyama vya watu stadi kupiga kambi mbele ya makao makuu ya jeshi katikati ya mji mkuu Khartoum kuanzia Aprili 6. Kwa sasa anazuiliwa kwenye gereza la Kober.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles