ADAM MKWEPU NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Al Ahly umekamilisha maandalizi yote muhimu ya timu yao kabla ya kuvaana na Yanga Jumamosi hii Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo inatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ajili ya mchezo huo wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika.
Al Ahly, ambao ni vinara wa Ligi Kuu nchini Misri, wataumana na Yanga wakiwa na kumbukumbu ya kuwaondosha wapinzani wao katika michuano hiyo mwaka 2014.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Ufundi wa Klabu hiyo, Syed Abudl Hafeez kupitia mtandao wa www. Al Ahly.com, tayari Balozi wa Misri nchini, Yesser Shawwaf na naibu wake, Ahmed Abdul Rahim, wamekamilisha mikakati yote ya ushindi na mapokezi ya timu hiyo.
“Balozi wetu alikuwa akiifuatilia Yanga kwa ukaribu na ameweza kutupa taarifa zote za wapinzani wetu kabla ya kukabiliana nao.
“Nimeweza kukutana na viongozi wa Yanga na kupanga muda wa mazoezi na mambo mengi, lakini napenda kumshukuru Balozi wetu amekuwa pamoja na mimi tangu nilipofika nchini Tanzania Jumapili iliyopita,” alisema Hafeez.
Upande wake Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro, alilipasha MTANZANIA jana kuwa timu hiyo itawasili leo mchana kwa Shirika la Ndege la Qatar na kufikia kwenye Hoteli ya Kilimanjaro Hyatt.
“Wapinzani wetu watawasili kesho (leo) mchana na tayari tumewaandalia basi la kuwapokea, lakini gharama nyingine za hoteli wamejigharamia wenyewe,” alisema Muro.
Muro alieleza kuwa licha ya timu hiyo kuwasili leo mchana, hajaweza kufahamu idadi kamili ya watu watakaokuwa kwenye msafara huo.
Yanga, iliyoweka kambi ya siku nne Kisiwani Pemba, itarejea jijini Jumamosi asubuhi kwa ajili ya mchezo huo.