26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Akamatwa na kadi 90 za kupigia kura

Na Elias Msuya

MWANAMKE aliyetambuliwa kwa jina la Salome Mahala, amekamatwa hivi karibuni katika Kata ya Nsimbo Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, akiandikisha namba za kadi za kupigia kura.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, mwananchi wa kijiji cha Katumba wilayani humo, alisema Mahala alikamatwa Jumatatu asubuhi akiwa na kadi 93 alizokusanya kwa wananchi akidai anaandikisha wanachama wa CCM.

“Tumemkamata huyo mama na kumfikisha katika kituo cha polisi cha mkoa akiwa na kadi 93 alizokuwa akichukua kwa wananchi. Wengi hawaelewi, huo ndiyo mchezo unaofanywa na CCM kuiba kura,” alisema mwananchi huyo.

Alisema mama huyo, amekuwa akizunguka vijijini nyumba kwa nyumba na kudai ametumwa na Serikali kuhakiki taarifa za vitambulisho hivyo.

“Yule tunamjua, hana cheo chochote serikalini ila ni kada wa CCM anayewadanganya wananchi kuwa anafanya uhakiki wa vitambulisho vya kupigia kura,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhamiri Kidavashari alikiri kukamatwa kwa Mahala na kusema uchunguzi unaendelea.

Hata hivyo, Kamanda Kidavashari alimlaumu mgombea ubunge wa jimbo la Nsimbo kwa tiketi ya Chadema, Gerald Kitabu akisema anapotosha taarifa za tukio hilo.

“Ni kweli huyo mwanamke alikamatwa akiwa anaandikisha vitambulisho vya wapiga kura huko vijijini. Yule ni kiongozi wa Jumuiya ya Wanawake ya CCM, anasema alikuwa akihakiki wapiga kura wao,” alisema.

Alisema mwanamke huyo ameachiwa kwa dhamana na uchunguzi unaendelea.

Awali mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo hilo, Gerald Kitabu alidai kuwa licha ya mwanamke huyo kukamatwa, polisi mkoani humo imekuwa ikipendelea makada wa CCM.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva alisema tume haina taarifa za kuandiskishwa kwa namba za kadi za kupigia kura.

“Mpaka sasa hatuna taarifa hizo, tuna wawakilishi wetu mikoani na wilayani, wakituletea tutaeleza hatua za kuchukua,” alisema Jaji Lubuva.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles