23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

AJENGA NYUMBA KWA KUTUMIA MAHINDI, INALINDWA NA PAKA

Joseph Hiza na Mashirika

MAHINDI ni chakula muhimu na tegemeo la kaya nyingi duniani hasa katika mataifa yanayoendelea kutokana na unafuu wa bei, upatikanaji wake.

Mbali ya hilo ni lishe bora iliyo chanzo cha protini inayosaidia kupunguza utapiamlo, kuongeza kinga dhidi ya maradhi ya kudumaa kimwili na kiakili pamoja na uwezo wa kufikiri.

Aidha hujenga mwili kutokana na wanga inayopatikana katika nafaka hizo ambazo huweza kutengenezwa unga.

Licha ya kuwa chakula bora ni zao zuri kibiashara kwa wakulima na pale linapopotea sokoni huwa kizaizai kwa familia na serikali nyingi kutokana na kuwa tegemeo.

Hivi karibuni katika mataifa mengi ya kusini mwa Afrika hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki yakiongozwa na Kenya, yalishuhuda serikali zikihaha namna ya kuziba pengo la uhaba lililotokana na ukame uliokumba sehemu nyingi mwaka juzi.

Uhaba wa mahindi pamoja na kupaa kwa bei kutokana na uhaba huo almanusura iingize matatani serikali ya Jubilee nchini Kenya baada ya kuonekana kuyumba kushughulikia tatizo hilo pamoja na kulenga kunufaisha washirika wao kibiashara katika utoaji vibali vya uingizaji mahindi.

Yote haya yanazungumzia kitu kimoja tu, mahindi ni muhimu sana katika maisha ya binadamu hasa mataifa masikini.

Lakini licha ya hilo, halikumzuia mwanaume mmoja wa China kuyatumia kinyume na matumizi halisi baada ya kujenga nyumba ya shambani kwa kutumia mahindi zaidi ya 30,000.

Malighafi hii ya ujenzi ya aina yake, yaani mahindi yakiwa hayajapukuchuliwa bado kutoka kwenye magunzi yake.

Liu Hongcai amejenga nyumba hiyo ya aina yake ya shambani karibu na jiji la Shulan katika jimbo la kaskazini mashariki la Jilin.

Alisaidiwa na wanakijiji 14 kuikamilisha nyumba yake hiyo ya ndoto yake.

Lakini hilo lilimgharimu kwani alitokwa na zaidi ya pauni 1,000 za Uingereza sawa na zaidi Sh milioni tatu za Tanzania kununulia mahindi 30,000 yaliyohitajika kwa mradi wake huo wa aina yake.

Nyumba hiyo ikiwa imekamilika, ikiwa na kisima, bustani na uzio vyote vikitengenezwa kwa malighafi hiyo ya mahindi– ilimchukua wiki mbili kuitengeneza na kuikamilisha Novemba 8 mwaka huu.

Ukiachana na malighafi zilizotumika kuijenga, muundo wa nyumba hiyo, ambayo bado haina fenicha umetokana na nyumba zinazopatikana eneo hilo.

Liu ameripotiwa akitumaini kuwa nyumba hiyo itawavutia watalii kuja eneo hilo.

Ikiwa na urefu wa futi 40 na upana wa futi 13, mbali ya kutumia malighafi za mahindi pia imetumia fremu zilizotokana na mbao na chuma. Mahindi hayo yameambatanishwa katika fremu hizo.

Lakini awali Liu, alihofia utumiaji wa mahindi, ulimaanisha kukaribisha panya kula nyumba yake hiyo, kabla ya ndoto zake kutimia au watalii kuiona.

Ili kukabiliana na tatizo hilo, mkulima huyo akaomba msaada wa paka kutoka eneo hilo kwa ajili ya kuilinda dhidi ya panya, kitu ambacho amefanikiwa.

Kwa sababu hiyo, hadi sasa waliopata hifadhi katika nyumba hiyo ni jeshi dogo la wanyama wa jamii ya paka, waliokimbia baridi kali la kaskazini mwa China, anasema naibu mkurugenzi wa ujenzi wa kijiji hicho, Yan Xue.

Alikaririwa akisema: “tumeleta paka wengi waliokuwa wanaranda randa mjini.

“Itawapatia nyumba. Nadhani hii ni wazo zuri kuwa nao kwa ajili ya kuilinda dhidi ya panya na wanyama wengine waharibifu,”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles