Elizabeth Kilindi -Njombe
ASKARI Polisi watatu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Njombe, waliokuwa wanakwenda kazini, wamefariki dunia huku tisa wakijeruhiwa.
Walifariki dunia baada ya gari lao lenye namba za usajili PT 3437 kugongwa na basi la abiria la Kampuni ya Sharon lenye namba za usajili T 349 CXB linalofanya safari zake Njombe – Arusha.
Akithibitisha kutokea tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamis Issah alisema tukio hilo lilitokea Febuari 3, mwaka huu saa 12:05 asubuhi, wakati gari la abiria lilipokuwa linashuka mteremko mkali kwenda Makambako.
“Gari hili lilikuja kwa mwendo kasi na kugonga gari la polisi waliokuwa wanaenda kazini kwenye malindo mbalimbali, ikiwamo nyumba za viongozi.
“Kilichotokea basi hilo liligonga bodi ya gari ambalo polisi walikuwa wamebebwa na bodi hilo liliweza kufumuka na kusababisha majeruhi kwa askari ambao wako nyuma mwa hilo bodi wapatao 11, walipelekwa Hospitali ya Kibena na askari watatu walifariki kabla hawajapata matibabu,” alisema Kamanda Issah.
Alisema basi hilo baada ya kugonga gari la polisi, liliendelea na mwendo kasi kuelekea maeneo ya bondeni sehemu ya Mto Ruhuji, barabara ya Makete na likashindwa kupanda mlima na basi hilo lilirudi na kubakiza nusu mita litumbukie mtoni.
Kamanda Issah alisema Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka dereva wa basi la Sharon ambaye alikimbia baada ya ajali kutokea.
Alisema hadi jana, wamemkamata mmiliki wa gari hilo ambaye yuko mkoani Arusha ili aweze kutoa anuani ya dereva wake.
“Kulisikika mwanzoni gari ili lina matatizo ya breki na gari hilo liliweza kuendeshwa na liliweza kusimama mpaka eneo la ajali, gari hili lina breki nzuri isipokuwa mwendo kasi, niwasihi madereva wanaokwenda asubuhi Dar es Salam muda huo sio wa mashindano eneo la mteremko huu, ni mkali,” alisema Kamanda Issah.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni askari namba H 4401 Marianu Hamis mkazi wa Mkoa wa Lindi, H 6802 PC Maiko Mwandu mkazi wa Mkoa wa Geita na H 7486 PC Hery Soko.
Askari majeruhi ni Saidi Mustafa, Mohamed Abdallah, Jeremiah Mwasapile, Abeid, Shabani Jumanne, Ally Ibrahim, Edward Joseph, Ally Rashid na Dickson Manyinjo (31).
Kamanda Issah alisema jeshi hilo linafanya taratibu za haraka kumsafirisha kwa ndege askari Dikson Manyinjo kwenda Taasisi ya Mifupa na Tiba ya Mgongo na Mishipa ya Fahamu (Moi) kutokana na kujeruhiwa vibaya maeneo ya shingo na mwilini.
“Majeruhi mmoja amepewa rufaa ya kwenda kutibiwa Muhimbili, hawezi kupanda gari labda usafiri wa ndege, sasa tunafanya utaratibu ili askari huyu asafirishwe kupelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi,” alisema Kamanda Issah.
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Mkoa wa Njombe, Alto Mtega alithibitisha kupokea majeruhi 12, huku askari watatu wakifariki dunia.
Mmoja wa majeruhi, Saidi Mustafa alisema aliona ghafla gari imegongwa kwa nyuma na kushindwa kutambua kilichoendelea.
Miili ya askari hao inatarajiwa kuagwa leo viwanja vya Jeshi la Polisi mjini hapa.