ADDIS ABABA, Ethiopia
FAMILIA zilizopoteza ndugu katika ajali ya ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia, zimeanza kukabidhiwa shehena ya majivu ili wafanye maziko kama ishara ya kuwaenzi waliofariki dunia.
Kwa mujibu taarifa zilizopatikana mjini hapa, maofisa walianza kutoa vifurushi vya majivu hayo jana yaliyokusanywa kutoka eneo la ajali kwa familia za abiria 157 pamoja na wafanyakazi wa ndege, kufuatia shughuli ya utambuzi wa mabaki ya miili kuchukua muda mrefu.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa uchunguzi wa vinasaba umeanzishwa kwa lengo la kutambua mabaki ya miili iliyopatikna, lakini wataalam wanasema unaweza kuchukua muda wa miezi sita.
Shirika la Habari la Ufaransa AFP, liliripoti kwamba familia za waliokufa katika ajali hiyo kutoka mataifa 35 zinapewa kiasi cha kilo mbili za majivu.
Shirika hilo liliripoti kwamba ibada ya kuwaombea waliopoteza maisha ilifanyika jana mjini hapa.
Shirika la Habari la Marekani, AP nalo liliripoti kwamba familia hizo zilipewa mifuko hiyo yenye uzito huo wa kilo mbili kwa ajili ya kufanya mazishi hayo ya wapendwa zao.
“Tumepewa majivu haya baada ya kazi ya utambuzi wa mabaki ya ndugu zetu kushindikana,”alisema mmoja wa wanafamilia hao.
“Hatutapumzika hadi tupewe mwili halisi au sehemu za mwili ya wapendwa wetu,”aliongeza mwanafamilia huyo.
Ndege hiyo ya Shirika la Ethiopia Airlines aina ya Boeing 737 Max 8 ilianguka Jumapili iliyopita dakika chache baada ya kuruka kutoka Uwanja wa ndege mjini hapa ikiwa safarini kuelekea Nairobi Kenya na kuua watu wote waliokuwemo.