Na Safina Sarwatt, Hai
ASKARI saba wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, wamejeruhiwa katika ajali mbaya iliyohusisha gari la jeshi hilo na lori kubwa la mizigo aina ya Volvo, lililokuwa likitoka Arusha kwenda Kilimanjaro.
Ajali hiyo ilitokea juzi, saa 1:30 asubuhi maeneo ya kwa Msomali Bomang’ombe Wilaya Hai katika barabara kuu iendayo Arusha –Moshi, ambapo gari la polisi lilikuwa likienda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alikiri kutokea kwa ajali hiyo.
Alisema gari la polisi, liligongwa na lori la mizigo iliyokuwa ikitokea Arusha, baada ya dereva wa gari hilo kushindwa kuhimili usukani na kuhama upande kulia.
“Askari wetu walipata ajali mbaya iliyowasababishia majeraha sehemu mbalimbali za miili yao, jambo la kumshukuru Mungu hakuna kifo…walikimbizwa Hopitali ya Rufaa ya KCMC kwa ajili ya matibabu,” alisema.
Alisema kati yao, wawili waliumia zaidi na watano hali zao si mbaya wametibiwa na kuruhusiwa.
Alisema chanzo cha ajali hiyo, ni uzembe wa dereva wa gari kubwa la mizigo ambaye alibana zaidi upande wa kulia wa barabara, hali ambayo ilisababisha kugonga gari la polisi.
“Namba za magari yote mawili tumezihifadhi kwa sababu za kiusalama, uchunguzi ukikamilika dereva aliyesababisha ajali atafikishwa mahakamani,”alisema.