WATU sita wamefariki dunia papo hapo na wengine zaidi ya 38 kujeruhiwa vibaya,baada ya basi walilokuwa wakisafirika kutoka Mwanza kwenda mkoani Iringa kupinduka juzi usiku.
Basi hilo lilipinduka katika eneo lenye mteremko mkali la Ipogolo baada ya dereva kushindwa kulimudu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa,Peter Kakamba alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 3:30 usiku baada ya basi la Lupondije la Scania mali ya Lupondije Express kupinduka eneo la mteremko wa Ipogolo lilipokuwa likielekea kushusha abiria wa kwenda mkoani Mbeya.
Alisema majeruhi 38 walifikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa na 11walitibiwa na kuruhusiwa, wakati 27 hali zao hazikuwa nzuri.
Mmoja wa abiria kwenye basi hilo, Wema Zuberi alisema mwendo wa basi hilo tangu linaondoka mkoani Dodoma ulikuwa wa kawaida.
Alisema baada ya kuingia Iringa mjini, dereva wa basi hilo alianza kuendesha kwa mwendo kasi na kusababisha abiria kulalamikia mwendo huo.
“Abiria wengi walionyesha kumlalamikia dereva kutokana na kuwapitisha vituoni kuwashusha huku akiendesha mwendo kasi,”alisema.
Alisema kabla ya kufika eneo la ajali ,dereva alishindwa kulimudu basi hilo kutokana na mteremko mkali, huku breki zake zikishindwa kufanya kazi.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Banenda Helen (45), Mbuyi Leoni (52) wote raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jojina Nyamboko (26) mkazi wa Songea,Magambo Masunga (51) mkazi wa Mwanza,Felister Mwinuka (19) mkazi wa Njombe, Tubilisiusy Selestine(33),Said Kitonyi (17),Richard Bett (33) raia wa Kenya na Jofa Abonga (30)mkazi wa Geita.
Wengine ni Victor Lameck (25), mkazi wa Kagera, Pius Samwel (20) mkazi wa Mara, Michael Hadu (46) mkazi wa Madaba Songea, Hassan Mfaume (20) kutoka Iringa, Heriet Mwitinda (29) mkazi wa Arusha, Kiliana Kalinga
(22) mkazi wa Mbeya, Hima Kifyasi (32) mkazi wa Bariadi, Omary Hassan (35) mkazi wa Makambako,Zuo Pawa (30) mkazi wa Mbeya, Chacha John (26) kutoka Iringa.
Wengine ni Timoth Sichoni (24) mkazi wa Dodoma, Ishimwe Jasmin (9) raia wa Rwanda, Mkagasana Sarafina (41) raia wa Rwanda, Zaina Kisaka (26) mkazi wa Manyara, Sara Sichone (26) mkazi wa Mwanza, Ivon Magaiwa (22)mkazi wa Mafinga, Solomoni Angolisye (58) mkazi wa Dodoma, Ivan Huwen (33) na mwingine ambaye hajatambuliwa kutokana na hali yake kuwa mbaya.
Alisema baada ya kutokea ajali hiyo dereva alikimbia.
Akizungumza eneo la tukio, Mkuu wa wilaya ya Iringa,Richard Kasesela alisema kazi ya kutafuta miili zaidi iliyobanwa na basi hilo imekuwa ngumu kutokana na kukosekana gari la kuinua basi hilo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Robert Salim alikiri kupokea miili ya marehemu sita na majeruhi 38.